Mwenyekiti wa Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Singida, Michael Madirisha akizungumza katika kikao cha mkutano mkuu wa vyuo hivyo ulioketi mjini hapa leo. Kulia ni Katibu wa Seneti, Paul Dotto na kushoto ni Katibu Hamasa wa Seneti hiyo , Amina Mussa.
Mkutano ukiendelea.
Spika wa Bunge la Serikali ya Wanafunzi ( TIASO) Taasisi ya Uhasibu Tanzania ( TIA) Kampasi ya Singida, Salim Salim akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Singida, Vedastus Nkonya, akizungumza kwenye kikao hicho. |
Na Dotto Mwaibale, Singida
VIJANA wa Vyuo na Vyuo Vikuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida wamesema kwamba wakati huu si wakutafuta katiba mpya bali ni kufanya kazi za kuiletea nchi maendeleo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu mkoani hapa Michael Madirisha wakati akizungumza katika kikao cha mkutano mkuu wa vyuo hivyo ulioketi mjini hapa leo.
” Suala la katiba ya nchi ni matakwa ya wananchi na sio kundi dogo itakapofika mahali ambapo wananchi tunaihitaji na Serikali itakapoliona hilo italifanyia kazi,”. alisema Madirisha.
Alisema kama vijana wa Vyuo na Vyuo Vikuu wa CCM kwa sasa ajenda yao ni maendeleo hivyo wanawaomba vijana wenzao wa Baraza Kuu la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) popote pale walipo waende kuungana nao ili wapaze sauti ya pamoja ya maendeleo.
Alisema vijana wanao wajibu wa kulitumikia Taifa na Taifa lolote lina imani na vijana hivyo wanakazi kubwa kuhakikisha linapata maendeleo.
Alisema vijana wanapaswa kuwa wazalendo wa nchi na kufanya kazi kwa bidii badala ya kukaa vijiweni wakipiga kelele na kutumiwa vibaya na wanasiasa.
Madirisha alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ndani ya nchi yetu.
Alisema katika kipindi cha uongozi wake ndani ya siku 100 Rais Samia Suluhu Hassan ameweza kukutana na makundi mbalimbali kama wazee, vijana, wanawake kwa lengo la kujua changamoto walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi.
Madirisha pia alimpongeza Rais kwa kuondoa asilimia sita kwenye mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kuendelea kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha nne.
“Nimpongeze tena Rais wetu kwa kuendelea kuwaamini vijana ambapo tumeona akilienzi jambo hilo kwa kuwateua na kuwapa nafasi mbalimbali za kiutumishi ndani ya Serikali na kuweka bajeti bora ambayo imelenga kuwanufaisha watanzania wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu ambapo katika suala la mikopo imetenga Sh.570 Bilioni kwa ajili ya wanufaika wa vyuo Vikuu kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Alisema mambo haya yanayofanywa na Serikali ndiyo yanayotakiwa kusifiwa na vijana.
Alisema anaipongeza Serikali kwa kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu tozo za mihamala ya simu suala ambalo limewagusa watanzania wengiwa hali ya chini ambalo linafanyiwa kazi hivyo kuja na majibu.
Akichangia kwenye kikao hicho Rais wa Serikali ya Wanafunzi ( TIASO) Taasisi ya Uhasibu Tanzania ( TIA) Kampasi ya Singida , Hamisi Ibrahim alisema kuhusu katiba mpya hadhani kama ni ya muhimu kwa sasa kwani katiba iliyopo imetutoa mbali na haina changamoto yoyote akitolea mfano tukio la nchi yetu kufiwa na Rais aliyekuwepo madarakani kwa mara ya kwanza ambapo tukiangalia nchi za wenzetu Rais anapokufa au hata kujiuzulu matatizo hutokea tofauti na hapa kwetu na ni katiba hiyo tulionayo ndiyo imetuvusha katika vipindi mbalimbali.
Alisema ni wajibu wa vijana kujitambua na kutumia akili zao kwa sababu wanaoshawishiwa kushiriki kwenye makongamano hayo ya kudai katiba ni vijana hivyo wana kazi kubwa ya kuelimishana.
Akizungumzia suala la uzalendo alisema ni changamoto kubwa kwani ndio chanzo cha rushwa, kuisemea nchi vibaya hivyo alitoa mapendekezo kwa seneti hiyo kuanzisha madarasa ya kufundisha watu kuhusu uzalendo.