Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa, kwa pamoja watazindua Studio za Redio jamii ya TBC Jumatatu Julai 26, 2021 katika jiji la Dodoma.
Ujenzi na ufungaji wa vifaa vya Kisasa katika Studio hizo umefadhiliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote( UCSAF) kwa lengo la kuboresha usikivu wa Radio Kanda ya Kanda.
Hayo yameelezwa leo katika mkutano na waandishi wa Habari uliofanywa na TBC kwa kushirikiana na UCSAF.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo, Julai 24, 2021 ikiwa ni maandalizi ya uzinduzi huo, Mtendaji Mkuu wa UCSAF amesema lengo la kufadhili ujenzi wa Studio hizo ni kuhakikisha kuwa wananchi wa pembezoni wanapata huduma ya mawasiliano ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa Mfuko huo.
“Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) na TBC tumeendelea kushirikiana kutekeleza miradi ya upanuzi wa usikuvu wa Mawasiliano wenye lengo la kupeleka huduma ya habari kwa wananchi kwa njia ya redio” amesema Justina.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayoub Rioba Chacha amesema kuwepo kwa Redio hiyo, kutasaidia katika kurusha habari za kikanda ili kukuza uelewa wa wananchi kuhusiana na masuala ya kijamii katika maeneo yao
Pia ameongeza kuwa radio hiyo itaongeza uwezo wa kuandaa vipindi vinavyohusu matukio ya kitaifa ikiwemo vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kurusha vipindi vya runinga kutokea Dodoma ikiwemo vipindi vya Jambo Tanzania na TBC Aridhio.
Ukarabati wa studio hizo pamoja na ufungaji wa mitambo ya kisasa kwa radio hiyo yenye masafa ya FM umegharimu kiasi shilingi bilioni 1.
Katika mwaka wa Fedha 2017/ 2018 UCSAF kwa kushirikiana na TBC walitekeleza mradi kama huo katika Mkoa wa Arusha kwa gharama ya shilingi milioni 627.
Miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ni pamoja ujenzi wa mitambo ya masafa ya FM katika wilaya za Ngara, Kyela, Ruangwa, Kilombero, Ludewa, Makete, Uvinza, Mbinga na Ngorongoro.
Mitambo mingine kama hiyo itafungwa katika studio za TBC Kanda ya Mwanza, Lindi, Songea, Kigoma na Mbeya.