Adeladius Makwega Chamwino- WHUSM
Serikali imewapongeza wadau wote wanaoandaa matamasha mbalimbali ya sanaa na utamaduni kwani kwa kukufanya hivyo kunakuza kulinda na kurithisha utamaduni wa Mtanzania.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamdauni , Sanaa na Michezo Mheshimiwa Innocent Bashungwa alipowakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bi. Leah Kihimbi katika kufunga Tamasha la Cigogo Chamwino Mkoani Dodoma.
Amesema kuwa Wizara itaweka mikakati thabiti kuhakiksha Tamasha la Cigogo linakuwa kubwa kama matamasha makubwa mengine yanayofahamika Kitaifa na Kimataifa.
Waziri Bashungwa amewaagiza wataalamu wa wizara yake kuhakikisha maombi ya Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa Chamwino na yale ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka yanatekelezwa kwa haraka na tamasha lijalo liwe kubwa na la mfano.
Awali kabla ya kuhitimisha tamasha hilo Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa Chamwino Dkt Kedmon Mapana aliomba Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kusaidia kufanikisha Tamasha la Cigogo la 13 kwa mwaka 2022.
Tamasha hilo lilipambwa na wasanii kuimba nyimbo zenye maudhui ya aina mbalimbali lakini kubwa kuliko yote ni nyimbo za Uviko 19 kutia fola.
Korona hauna huruma,
Mbona utumaliza,
Mbona unatutesa,
Amani haipo tena,
Korona korona ehh
Kazi nyingi zimesimama
Uchumi umeshuka
Tatizo ni korona
Bado unatusumbua.
“Ni kweli tulijitahidi kuhakikisha ugonjwa huu wa Uviko 19 unaeleweka kwa hadhira yetu ambayo kwa muda wa siku mbili ilikuwa ikitega masikio na kukodolea macho yao kwenye ngoma zetu za kitamaduni kama huo wimbo ulioimbwa na Kikundi cha Nyota Njema Chamwino.” Amesisitiza Dkt Kedmon Mapana.
Tamasha hilo la Cigogo limetamatishwa kwa wasanii kuonyesha sanaa zao za maonesho ikiwemo ngoma za makabila mbalimbali.