Mchezaji wa kati wa TAMISEMI QUEENS Sophia Komba akijaribu kumhadaa mchezaji Bahati Mabula wa Magereza katika mchezo mkali na wa kusisimua wa netiboli ligi daraja la kwanza ambapo TAMISEMI QUEENS walishinda mchezo huo kwa magoli 49-35.
Mchezaji Semeni Abeid wa TAMISEMI QUEENS akikimbia na mpira kuelekea goli la Magereza ya Morogoro huku akichungwa kwa karibu na ‘senta’ wa Magereza Bahati Mabula katika mchezo mkali na wa kusisimua wa netiboli ligi daraja la kwanza ambapo TAMISEMI QUEENS walishinda mchezo huo kwa magoli 49-35.
Kocha wa TAMISEMI QUEENS Maimuna Kitete akibadilishana mawazo na Mmoja wa Viongozi Wakuu wa TAMISEMI QUEENS Rose Makange mara baada ya mchezo mkali na wa kusisimua wa netiboli ligi daraja la kwanza kati ya TAMISEMI QUEENS na Magereza ya Mrogoro ambapo TAMISEMI QUEENS walishinda mchezo huo kwa magoli 49-35.
******************************
Na Mathew Kwembe, Arusha
Timu ya Netiboli ya Maafande wa Jeshi la Magereza ya mkoani Morogoro leo imesalimu amri kutoka kwa Mabingwa wa Netiboli wa Ligi ya Muungano wa mwaka 2019, timu ya TAMISEMI Queens ya Dodoma baada ya kukubali kipigo cha magoli 49-35.
Hadi robo ya kwanza ya mchezo inamalizika TAMISEMI QUEENS walikuwa mbele kwa magoli 13-5, na katika robo ya pili na ya tatu TAMISEMI QUEENS waliongoza kwa magoli 23-14, na 34-25.
Katika robo ya pili kocha wa Magereza alimtoa Mshambuliaji Naima Boli na kumuingiza Mwanaasha Ally, mabadiliko ambayo yalileta uhai kwa timu ya Magereza kwani mchezaji huyo alionyesha uhai kwa timu hiyo na kuwapa wakati mgumu walinzi wa TAMISEMI QUEENS.
Katika mchezo huo, wachezaji Semeni Abeid na Sophia Komba waliweza kushirikiana vema katika dimba la katikati na kusababisha hatari za mara kwa mara katika goli la maafande wa Magereza.
Magoli ya Magereza yalifungwa na wachezaji Naima Boli, Mwanaasha Ally na Mary Msangi huku wafungaji wa TAMISEMI QUEENS ni Lilian Jovin na Aziza Itonye.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo Mlinzi wa pembeni wa TAMISEMI QUEENS Mersiana Kizenga alisema kuwa timu yake ilipambana ili kupata ushindi huo.
Mchezaji huyo ambaye ndiye aliyekuwa anaanzisha mashambulizi dhidi ya Magereza alisema kuwa mchezo wa leo ulikuwa mzuri na kila timu ilikuwa ikitafuta ushindi ndiyo maana alilazimika kufanya kazi ya ziada ya kutibua mipango ya wachezaji wa Magereza kila walipo karibia goli la TAMISEMI QUEENS.
Kufuatia ushindi huo TAMISEMI QUEENS chini ya kocha wake Maimuna Kitete imeendelea vema na kampeni yake ya kutwaa ubingwa wa ligi ya Netiboli nchini ambao unashikiliwa na timu ya JKT Mbweni ya Dar es salaam.
Hadi sasa TAMISEMI QUEENS ambayo ndiyo timu pekee kutoka katika wizara inayoshiriki ligi daraja la kwanza, imeshinda mechi zake zote nne sawa na timu ya JKT Mbweni
Kesho timu ya TAMISEMI QUEENS itacheza michezo miwili katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo ambapo asubuhi itapambana na maafande wa JKT Mgulani na mchana timu hiyo inayomilikiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI itacheza dhidi ya timu ya Uhamiaji ya jijini Dar es salaam.
Matokeo mengine ya michezo iliyochezwa jana na leo inaonyesha JKT Mbweni imeichapa Uhamiaji magoli 61-40, Polisi Arusha imeifunga Arusha Jiji magoli 55-22, Ihumwa Dream Team iliigalagaza Polisi Arusha magoli 46-44, na Magereza Morogoro imeichapa JKT Mgulani magoli 39-35.