…………………………………………………………………..
Adeladius Makwega
WHUSM –Dodoma.
MWANAMUZIKI Waziri Ali Seifu maarufu kama Waziri Njenje amefariki dunia Julai 23,2021 katika Hospitali ya Mwananyamala Jijini Dar es Salaam.
Kulingana na taarifa zilisombaa katika vyombo mbalimbali vya habari na kuthibitishwa na katibu Mkuu wa Chama Cha Muziki wa Dansi nchini (CHAMUDATA), Hassani Msumari amesema ni kweli mwanamuziki huyo amefariki na msiba upo nyumbani kwa marehemu nyuma ya Duka la Dawa la Nakiete Mwenge mwisho Jijini Dar es Salaam.
Kulingana na taarifa zilizokusanywa juu ya mwanamuzi huyo, imefahamika kuwa aliweza kufanya kazi ya sanaa ya muziki kwa zaidi ya miaka 50 na miaka 44 pekee hadi anafikwa na umauti amekuwa ni msanii na kiongozi wa bendi ya The Kilimanjaro Band.
“Leo ni siku ya Jumamosi kwa desturi yake Waziri Ally alikuwa akiamka asubuhi na kufanya shughuli zake za kawaida na ikifika jioni anarudi hapa nyumbani kwa mapumziko ili kujiandaa na maonesho yake ya usiku katika kumbi mbalimbali za burudani akiwa na wananjenje-The Kilimanjaro Band.” Alidokeza Masoud Masoud ambaye ni Mtangazaji Mkongwe wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na mdau mkubwa wa muziki nchini.
Sasa hatunaye tena, ndiyo ameondoka, kubwa kwa wanamuziki wa Kitanzania ni kuiga mema ya ndugu yetu Waziri, haswa la kuweza kuwaunganisha wanamuziki na kuweza kuwafundisha vijana wengi muziki husasani upigaji wa ala za muziki ameongeza Masoud Masoud.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mfaume Said, amesema kuwa amepokea kwa masikitiko msiba huo kwani mchango wa Waziri Ally ni mkubwa na hauna kipimo cha kupimia.
“Kumuenzi ni kuyaiga mazuri yake na kuendelea kukuza sanaa ya muziki nchini kwa manufaa ya kizazi cha leo na kijacho.”Aliongeza Kaimu Mkurugenzi huyo.
Mwaanamuziki Waziri Ally ni mzaliwa wa Pongwe Tanga ataendelea kukumbukwa na wadau wa muziki na Watanzania wengi kwa nyimbo kadha wa kadha kama vile Kinyanyau, Tupendane Mpenzi , Gere na nyingine nyingi.
…”. Mie na wangu nyumbani,
Mambo yangu Burudani,
Masikio nimeziba,
Sijali ya mitaani,
Wangu nimedhibiti,
Hasiki wala haoni,
Jaribuni Kwengine,
Hapa hamuoni ndani,
Wacha wachawaseme , watasema mchana ehh na usiku watalala .”
Kwa hakika Waziri Ally ametutoka , huu ni wakati mgumu kwa familia, wakati mgumu kwa wapenzi wake wa muziki na wakati mgumu kwa CHAMUDATA na sisi Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulikisikia.” Kwa hakika maneno hayo ya Kitabu kimojawapo cha dini yanaufunga ukurasa wa maisha ya mwanamuziki Waziri Ally na ni kweli msiba ni neno gumu, Kwaheri Waziri Ally.