Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (Aliyesimama katikati kwenye Chuma) akizungumza katika eneo la ujenzi wa mnara wa TTCL katika kijiji cha Masenge Mamiwa Wilaya ya Gairo Morogoro wengine ni watendaji aliombatana nao na wananchi wa eneo hilo
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa kwanza kulia) akizungumza katika eneo la ujenzi wa mnara wa TTCL katika kijiji cha Masenge Mamiwa Wilaya ya Gairo Morogoro wakati wa Ziara yake ya kukagua miundombinu na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika Mkoa huo
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kulia mstari wa mbele) akizungumza wakati wa ziara yake katika mnara wa mawasiliano wa TTCL uliopo katika Kijiji cha Kiganira Morogoro vijijini. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya MorogoroVijijini Mhe. Albert Msando
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika kata ya Chakware iliyopo Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (Katikati aliyeshika kiuno) alipotembelea eneo ambalo lilitakiwa kuwa na mnara wa Halotel katika Kijiji cha Idibo wilayani Gairo lakini bado mnara huo haujajengwa. Anayefuata kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame. Kulia ni Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Mhandisi Albert Richard.
…………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, MOROGORO
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetakiwa kuonesha ushindani katika soko la mawasiliano nchini kwa kupanua wigo wa mtandao wake pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma zake za laini za simu, vocha, T- Pesa katika maeneo ya mijini na vijijini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu na ya msingi ya mawasiliano ya sauti na data
Akiwa katika ziara ya kukagua miundombinu ya mawasiliano na hali ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika Mkoa wa Morogoro Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa katika ziara alizofanya Mikoa ya Mtwara, Kilimanjaro na Tanga amekutana na changamoto za upatikanaji wa huduma za Shirika hilo wakati wananchi wanahitaji kutumia mtandao wa TTCL
Amesema kuwa tabia za wateja zinaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia kwa mfano matumizi ya data kuongezeka kwasababu ya mitandao ya kijamii na programu tumizi zinazotoa huduma za kijamii hivyo katika zama hizi za kidijitali Shirika la TTCL linatakiwa kwenda sambamba na mabadiliko ya tabia za wateja ili kuakisi mahitaji yao
“Shirika la TTCL mnatakiwa kuboresha na kuongeza wigo wa upatikanaji wa mtandao wenu na huduma zake badala ya kuweka uwekezaji mkubwa kwenye promosheni halafu wateja wakija hawapati huduma wanazostahili kuzipata”, alizungumza Mhandisi Kundo
Aliongeza kuwa ni kazi kubwa kumrejesha mteja ambaye Shirika litampoteza kutokana na kukosekana kwa huduma alizotarajia kuzipata hivyo kulitaka Shirika hilo kuboresha miundombinu yake ili huduma zake ziwe na uwezo unaokidhi mahitaji
“TTCL kuna Minara imejengwa na imekamilika lakini haijawashwa nendeni mkaiwashe, na ile ambayo ilikuwa tayari ipo kwenye mpango wa kujengwa ijengwe, inayotakiwa kuongezewa uwezo iongezewe, kwasababu hili ni Shirika la umma hivyo mnatakiwa kuwafikia wananchi katika maeneo yote hadi yale yasiyokuwa na mvuto wa biashara”, alizungumza Mhandisi Kundo
Aidha, amezungumzia huduma ya intaneti yenye kasi kuwa ni huduma ya msingi yenye mchango mkubwa wa kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kidijitali na kufanyika kwa biashara mtandao ambapo ni wajibu wa Serikali kupitia taasisi za mawasiliano kuhakikisha wananchi wake katika maeneo yote wanapata na kutumia huduma ya intaneti
Kwa upande wa wananchi waliojitokeza katika miradi ya minara ya mawasiliano ya TTCL iliyopitiwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri huyo wamesema kuwa wao wanahitaji kurudi nyumbani kwa sababu wanaambiwa kumenoga kama kauli mbiu ya Shirika hilo inavyosema “Rudi Nyumbani Kumenoga” hivyo wameomba kuboreshewa uwezo na ubora wa mtandao huo pamoja na huduma za vocha, laini za simu na T-Pesa kwasababu katika maeneo mengi hazipatikani na wakati mwingine wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma hizo
Katika ziara hiyo Naibu Waziri aliambatana na watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ikiwemo watendaji kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambapo walipokea maelekezo ya Naibu Waziri kuhusu kufuata utaratibu wa ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano katika vipengele vya ubora, uwezo, vibali vya ujenzi, mikataba ya ujenzi na ulinzi na mahitaji ya wananchi kwa ujumla wake na kuahidi kuwa Shirika litafanyia kazi maelekezo hayo kwa muda muafaka
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari