Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akifafanua jambo wakati akiongea na Waandishi wa habari kuhusu ufuatiliaji wa utekelezaji wa matamko yaliyotangulia kuhusu kupambana kudhibiti UVIKO-19, Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi akieleza jambo
***************************
Tarehe 23 Julai, 2021 Dar es Salaam.
Ndugu Wananchi, mtakumbuka kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikitoa matamko mbalimbali yanayolenga kuwataarifu na kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu kutekeleza afua za kujikinga na kuwakinga wengine juu ya UVIKO-19.
Mapema asubuhi leo nimefanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa matamko husika na kubaini kuwa bado katika baadhi ya maeneo kuna ulegevu. Aidha, wananchi kadhaa kupitia simu na ujumbe mfupi wa simu wamenifikia wakitaka ufafanuzi juu ya misongamano ipi hasa imekatazwa huku wengine wakitoa taarifa kuwa katika baadhi ya maeneo waliko viongozi wao wako kimya kama vile hakuna wanachotakiwa kufanya.
Ndugu Wananchi, nikiri kuwa baadhi ya maeneo nawaona Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wataalamu watendaji walio kwenye ofisi zao wakiwa mstari wa mbele kuhamasisha na kuelimisha na kuchukua hatua stahiki huku wananchi wakipokea na kutekeleza. Aidha, kwenye baadhi ya maeneo mengine ni kweli kuko kimya kama vile hakuna uongozi wala viongozi.
Ndugu Wananchi, nchi hii ina mfumo mzuri wa viongozi na uongozi wa serikali ngazi zote kuanzia Wizara, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa hadi Vijijini. Viongozi hawa ndiyo wenye dhamana ya kuongoza watanzania kila ngazi. Nichukue fursa hii kutambua na kuwapongeza sana viongozi hawa kwa kazi kubwa ambazo wamekuwa wakifanya na kulivusha taifa kwenye mambo mengi ikiwemo kuifikisha sekta ya afya kwenye mafanikio makubwa hapa ilipo leo.
Aidha, kwenye hili la kupambana na UVIKO 19 wako baadhi ya viongozi wanaofanya vizuri na wako baadhi ya viongozi ambao hawafanyi vizuri kwani wana kasi ndogo kwenye kusimamia utekelezaji wa maagizo na maelekezo yanayolenga kuwafanya wananchi washinde vita dhidi ya UVIKO 19 kwa haraka na kwa gharama ndogo.
Ndugu Viongozi na Wananchi, nawakumbusha tena kuwa tusifanye mzaha na UVIKO 19 na tusichukulie kwa wepesi tu kuwa mbona wimbi la kwanza na la pili lilipita na nipo. Jamii ya Virusi vinavyozunguka inabadilika na inatofautiana makali ya kushambulia hivyo usiupe kazi mwili wako unaweza kuchoka bila sababu na ukajikuta umeugua na au kufariki kabisa, pambana. Tatizo lipo na linagharimu watu uchumi na uhai. Ikiwa jana nilitangaza kuwa tarehe 21/07/2021 tulikuwa na wagonjwa waliolazwa 682 nchi nzima (ambao ndiyo tuliweza kuzifikia takwimu zao) kwa jana peke yake wagonjwa wapya waliolazwa kwa takwimu zilizotufikia walikuwa 176. Ikumbukwe hawa ndiyo walioripoti vituo vya huduma za afya na huenda wengine wako majumbani.
Vilevile, ikumbukwe kwamba siyo kwamba watu hawafariki la hasha wanafariki na kwa takwimu za tarehe 21/07/2021 waliofariki ni 29 kwa takwimu zilizotufikia. Itoshe kusema tatizo lipo, lazima tusimame tupambane bila kuathiri shughuli zetu za uchumi na kutiana hofu tukajikuta tumeongezea tatizo lingine.
Ndugu Viongozi na Wananchi, tunaposema tuzingatie kutekeleza afua za kujikinga na UVIKO 19 ni lazima wananchi watimize wajibu wao na viongozi wa wananchi nao watimize wajibu wao na utekelezaji uonekane bayana. Kila mmoja wetu awe mwananchi au kiongozi ajiulize, je anapofanya mambo kinyume na maelekezo ya kuchukua tahadhari analenga kumtesa nani? Mfano;
- Tunapojazana na kusongamana kwenye viwanja kuangalia burudani mbalimbali kama mpira au jambo lolote bila kuchukua tahadhari; kwani haiwezekani wakabaki wachache ikawezekana kuwamudu kutekeleza tahadhari? Na huyo anayekaribisha tu watu wengi na kuwafanya wasongamane pasipo uwezekano wa kutekeleza afua za kinga kwa ufanisi je anakuwa anayo nia gani?
- Tunapokusanyika kwenye mikusanyiko ya kisiasa, kijamii na kidini tukiwa tumesongamana na bila tahadhari yoyote hivi hao viongozi wa shughuli husika wanakuwa wamekusudia nini? Kwani hawawezi kuwa na idadi ndogo ya wawakilishi na wengine wakafuatilia kwa njia zingine za mawasiliano hata redio wakiwa majumbani kwao?
- Tunapojazana kwenye vyombo vya usafiri bila tahadhari na uongozi wa sekta husika ya uchukuzi wapo ngazi zote na sheria wanayo hivi wanakuwa wanakusudia nini?
- Tunapokuwa tunatoa huduma za kijamii zinazowaleta pamoja watu kadhaa kwenye huduma yako halafu hakuna tahadhari za kuvaa barakoa, kunawa kwa maji na sabuni au vitakasa mikono hivi tunakusudia nini mfano sehemu za ofisi za umma pamoja na stendi, masoko, maduka mbalimbali madogo na makubwa zikiwemo supermarkets?
- Tunapopanga kufanya matamasha na mabonanza makubwa makubwa kipindi hiki hivi tunatarajia nini? Kwamba kirusi kipya kitatuacha salama kama awali? Je wewe usiyekinga wengine utakuwa umefanikiwa kuvibeba bila kuugua na kuwaambukiza wangapi?
- Tunapoenda mnadani kupata huduma za kijamii bila tahadhari na tukaketi huko siku nzima tumesongamana kwani hatuwezi kwenda mnadani tukiwa tumejikinga na kuwakinga wengine na tukamaliza shughuli tuklarejea nyumbani?
Napenda kuuliza tu kuwa hivi haya yote tunayafanya kupuuza utekelezaji wa maelekezo tunakuwa tunasubiri nini kitokee ili tutekeleze kwa ufanisi?
Ndugu Wananchi na Viongozi, tumebaini ulegevu kwenye kutekeleza afua za kujikinga na kuwakinga wengine unachangiwa na baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali kutotimiza wajibu wao vilevile unachangiwa na wasemaji wasio rasmi ambao kazi yao ni kupotosha hivyo, viongozi na wananchi tuwe makini. Afya yako na uhai wako hauna dhamana na mwingine ambaye wala hajulikani yuko wapi.
Ndugu Wananchi na Viongozi, napenda kuweka wazi kuwa serikali haitaendelea kuvumilia kuona baadhi ya viongozi hawatimizi wajibu wao kwenye kusimamia mapambano dhidi ya UVIKO 19. Niweke wazi kuwa tunafuatilia utekelezaji wa maelekezo yote ya serikali na tukiona kuna ulegevu mahali hoja ya kila asiyetimiza wajibu itawasilishwa kwa mamlaka husika ya ajira na nidhamu ili sheria, taratibu na kanuni zihusike. Ikumbukwe kuwa vita ya UVIKO 19 ni ya kitaifa, kila mmoja na kila sekta inahusika kwa nafasi yake.
Ndugu Wananchi na Viongozi, Serikali ingependa kuona kila kiongozi anajitokeza kwa nafasi yake akifuatilia, kuelimisha na kufafanua kwa jamii juu ya umuhimu wa kutekeleza afua za kujikinga na UVIKO 19. Kuhimiza kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa, kutosongamana, kufanya mazoezi, kula lishe bora, kuwahi vituo vya kutolea huduma za afya haihitaji elimu maalumu ya afya na kama inahitajika wataalamu wa afya wanaweza kufikika na kila mamlaka ya ofisi za serikali. Hali siyo nzuri mimi ndiye Waziri wa Afya nawaeleza na siwatishi wala siwatii hofu huo ndiyo ukweli, tutimize wajibu wetu.
Ndugu Wananchi na Viongozi, Nawapongeza sana Wakuu wa Mikoa na Wilaya na watendaji wao wote wakiwemo wa sekta binafsi na viongozi wa dini ambao wameshaonesha bayana kuwa wako mstari wa mbele kwenye mapambano ya kudhibiti UVIKO-19. Niwatie moyo kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan inayo macho inawaona na kumuona kila mtu bila miwani.
Hivyo, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wataalamu wote wanaohudumu kwenye ofisi zenu hadi ngazi ya Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji wa Mitaa, Maafisa Tarafa, Viongozi wa Taasisi za Serikali na Taasisi Binafsi nawakumbusha tena elimisheni jamii na watumishi walio chini yenu juu ya kuzingatia utekelezaji wa afua za kujikinga na UVIKO 19. Miongozo ya Wizara kuhusu nini kifanyike ipo kwa wataalamu wa afya waliopo kwenye ofisi zenu. Matamko yote ya maelekezo na elimu yapo kwenu.
Ndugu Viongozi na Wananchi, kwa kusema haya Serikali haitarajii kuendelea kuona kuna udhaifu kwenye kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa afua za kujikinga na kukinga wengine dhidi ya UVIKO 19. Ikiwa wewe ni Kiongozi uliyepewa fursa na dhamana ya kutumikia jamii kwenye nafasi uliyopo sasa simamia utekelezaji wa maelekezo halali ya serikali yanayolenga kulinda ustawi wa wananchi wake. Hili siyo ombi ni lazima kutimiza wajibu huo kwa nafasi yako kama kiongozi na mengine wannachi watatimiza.
Nipende kusema kuwa, udhaifu wowote kwenye kusimamia utekelezaji wa miongozo, maelekezo na matamko itakuwa ni kielelezo cha kutosha kujenga hoja kwenye mamlaka ya ajira na nidhamu ya kila kiongozi husika ili mamlaka husika ione hatua zipi zinafaa dhidi ya hoja iliyowasilishwa. Utoaji taarifa za kasi ya maendeleo ya utekelezaji ni zoezi endelevu kuanzia sasa.
Ndugu Wananchi na Viongozi, nimalizie kwa kusema kuwa, wananchi wengi wamekuwa wakifuatilia kuuliza lini chanjo zinakuja. Niwahakikishie kuwa kesho tutawasilisha taarifa ya utaratibu wote wa jinsi gani huduma ya chanjo itapatikana. Aidha, kwa kuwa chanjo zilizopatikana ni za wamu ya kwanza kati ya awamu kadhaa zilizopangwa kuja, tumeweka utaratibu mzuri wa kuzitoa kwa vipaumbele vya makundi maalumu tukianzia na wale ambao wanakutana moja kwa moja na mgonjwa wakito huduma za kijamii pia wazee na makundi mengine ambayo kesho tutayataja.
Niwahakikishie kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita itahakikisha kila mtanzania kwa hiari yake na bila malipo anapata huduma ya chanjo kwa kadri zinavyopokelewa.