******************************
Na Munir Shemweta, MTWARA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kushiriki katika ziara za viongozi ili kuweza kujibu changamoto zitakazojitokeza wakati wa ziara.
“Kiongozi akija eneo lako hakikisha uko katika msafara kama suala la ardhi likijotokeza basi wewe uweze kutoa ufafanuzi ili hatua zichukuliwe” alisema Dkt Mabula
Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi mkoani Mtwara tarehe 23 Julai 2021, Dkt Mabula aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika mikoa kuhakikisha wanakuwa na daftari maalum la kuorodhesha migogoro ya ardhi na hatua zilizochukuliwa sambamba na kuandika taarifa kuhusiana na migogoro husika kwenda ofisi za wakuu wa wilaya.
“Kumekuwa na utaratibu akija kiongozi mpya migogoro inaibuka upya sasa mhakikishe migogoro hiyo inaandikwa kwenye mfumo wa matrix ili kmrahisishia kiongozi na kumuepusha kupokea malalamiko yaliyokwisha fanyiwa kazi.
Aidha, katika kuhamasisha wanachi kulipa kodi ya ardhi Dkt Mabula alizitaka halmashauri kuandika taarifa ya jinsi zilivyotoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama vile redio za kijamii.
Pia aliwaeleza watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Mtwara kuwa anafikiria namna ya kuanzisha ushindani wa ukusanyaji kodi ya ardhi katika halmashauri kwa lengo la kuona halmashauri iliyofanya vizuri zaidi.
katika kujenga nidhamu ya watumishi, Dkt Mabula aliagiza watumishi wa sekta ya ardhi kutotoka nje ya vituo vyao vya kazi bila wakurugenzi kuwa na taarifa na kusisitiza kuwa watumishi wa ardhi wanatakiwa kutatua migogoro na si kuwa sehemu ya migogoro.
Akielezea upangaji miji katika maeneo mbalimbali nchini Naibu Waziri wa Ardhi alisema, pamoja na Wizara kusaidia harakati za upangaji Upimaji na umilikishaji ardhi katika halmashauri lakini jukumu la upangaji linabaki kwa halmashauri kwa kuwa ndiyo mamlaka ya upangaji.
” Si jukumu la wizara kuingilia upangaji wa miji katika halmashauri ila inazisaidia kuzikopesha fedha na kueleza kuwa zipo halmashauri zilizopewa milioni 200 hadi 300 lakini zipo nyingine zimetumia fedha kwa mambo mengine na nasisitiza pesa ziende katika masuala ya ardhi” alisema Dkt Mabula.
Mmoja wa wananchi wa Mtwara Sheikh Nurdin Abdalaah Manguji anayemiliki takriban hekta 8.704 katika eneo la Shangani West Mtwara aliimuomba serikali kupitia wizara ya Ardhi kumsamehe kodi anayodaiwa miaka ya nyuma kwa kuwa hakuwahi kufahamishwa na kupatiwa nyaraka za eneo lake.