Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe.Halima Okash akisaini kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili Chuo Kikuu Mzumbe.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mvomero pamoja na Wajumbe wa timu ya Menejimenti ya chuo Kikuu Mzumbe wakiwa katika kikao cha pamoja na Mkuu wa wilaya alipozuru chuoni hapo
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka akitoa taarifa fupi kuhusu Chuo mbele ya Mkuu wa Wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe.Halima Okash akisikiliza kwa umakini taarifa ya chuo kutoka kwa Makamu Mkuu wa chuo
Makamu Mkuu wa Chuo Prof.Lughano Kusiluka (kushoto) pamoja na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia masuala ya fedha na Utawala Prof.Ernest Kihanga wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa wilaya Mhe.Halima akiagana na Makamu Mkuu wa Chuo kikuu Mzumbe
*****************************
Mkuu wa wilaya ya Mvomero Mhe.Halima Okash, kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa, amefanya ziara ya kikazi Chuo Kikuu Mzumbe na kukutana na timu ya Menejimenti ya chuo hicho iliyoongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof.Lughano Kusiluka.
Akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Mhe. Okash ameleza madhumuni ya ziara hiyo ni kujitambulisha pamoja na kuhamasisha taasisi zilizopo wilayani Mvomero kushiriki kikamilifu katika mbio za Mwenge wa Uhuru, utakaokimbizwa wilayani humo tarehe 08 Agosti, mwaka huu.
Amepongeza uongozi wa chuo hicho kwa historia yake nzuri Kitaifa, na kwamba kama Mkuu Wilaya anajivunia chuo hicho kuwepo ndani ya wilaya anayoiongoza. Amesema Chuo Kikuu Mzumbe kimekuwa na historia nzuri ya kuzalisha Viongozi mahiri na wenye weledi mkubwa katika uongozi yeye akiwa mmoja wapo wa zao la Mzumbe.
Ameahidi kuendelea kukiwakilisha vema chuo hicho katika uongozi wake kwa kushirikiana kwa karibu na uongozi na Menejimenti ya Chuo hicho, na wanataaluma kuwaletea maendeleo wananchi wa Mvomero.
Akizungumza katika kikao hicho Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lughano Kusiluka, amesema Wanajumuiya ya Chuo Kikuu Mzumbe wanayo furaha kubwa kuongozwa na kiongozi waliemuandaa na kwamba watampatia ushirikiano unaohitajika kama ilivyokuwa kwa Viongozi waliotangulia, na kusisitiza kwamba Mzumbe ni Mdau mkubwa wa Maendeleo wilayani Mvomero kwa kuzingatia wajibu wake wa kitaifa wa kutoa elimu na kuihudumia jamii kama kauli mbiu yake inavyosema “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu” .