Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 21,2021 kuhusu wiki ya PASS Trust inayotarajia kuanza kesho Julai 22 hadi 24 mwaka huu itakayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa PASS Trust Anna Shanalingigwa,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 21,2021 kuhusu wiki ya PASS Trust kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameandaa wiki hiyo inayoanza kesho Julai 22 hadi 24 mwaka huu katika viwanja vya Nyerere Sguare jijini Dodoma.kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri
Kaimu Mkurugenzi wa PASS Trust Anna Shanalingigwa,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo Julai 21,2021 kuhusu wiki ya PASS Trust kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameandaa wiki hiyo inayoanza kesho Julai 22 hadi 24 mwaka huu katika viwanja vya Nyerere Sguare jijini Dodoma.
…………………………………………………………………
Na Alex Sonna,Dodoma
TAASISI ya PASS Trust (Private,Agriculture Sector Support Trust imeandaa wiki ya PASS Trust itakayowakutanisha wakulima,wauza zana za kilimo,taasisi za kifedha,wauza pembejeo,viongozi wa Serikali na wachakataji katika kuzungumzia maswala ya upatikanaji wa fedha kama kichocheo cha ukuaji wa kilimo biashara.
Akizungumza leo Julai 21,2021 na Waandishi wa Habari,Kaimu Mkurugenzi wa PASS Trust Anna Shanalingigwa amesema kuwa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameandaa wiki ya PASS Trust inayoanza kesho Julai 22 hadi 24 mwaka huu katika viwanja vya Nyerere Sguare jijini Dodoma.
Bi.Shanalingigwa amesema wiki hiyo itawakutanisha wakulima,wauza zana za kilimo,taasisi za kifedha,wauza pembejeo,viongozi wa Serikali na wachakataji katika kuzungumzia maswala ya upatikanaji wa fedha kama kichocheo cha ukuaji wa kilimo biashara.
Amesema kuwa watawapa fursa ya kipekee wakulima kuweza kuzungumzia changamoto mbalimbali wanazokutana katika kusaka mitaji ambapo pia Taasisi mbalimbali za kifedha watazungumza kuhusu upatikanaji wa mikopo.
“Wadau na wanufaika wa PASS Trust watapata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu huduma zetu pamoja na kukutana na kubadilishana mawazo ya kuboresha kilimo biashara nchini,”amesema Bi.Shanalingigwa
Katika hatua nyingine,Kaimu Mkurugenzi huyo amesema siku ya kilele Julai 24 mwaka huu,Waziri wa Kilimo,Mh.Prof.Adolf Mkenda anatarajiwa kuzindua kampuni mpya ya PASS Leasing Company LTD inayomilikiwa na Taasisi ya PASS Trust yenye lengo la kutoa mikopo ya zana za kilimo bila dhamana yoyote.
“Kampuni hiyo mpya tayari imeanza kutoa huduma zake za mikopo ya zana za kilimo inawawezesha wakulima wadogo,wa kati,wakubwa,na vikundi mbalimbali vinavyojishughulisha na shughuli zote zinazoendana na kilimo katika mnyororo mzima wa thamani, kuweza kumiliki vifaa hivyo bila kuweka dhamana yoyote,”amesema.
Akizungumzia PASS Trust,Bi.Shanalingigwa amesema kuwa ilianzishwa na Serikali ya Tanzania na Denmark miaka 20 iliyopita kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha na kibiashara kwa wajasiriamali wa bidhaa na huduma katika sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi nchini.
Amesema lengo kuu la Taasisi hiyo ni kupunguza umaskini nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wakulima kupitia udhamini.
“PASS inatoa dhamana ya mikopo kuanzia asilimia 20 -60( hadi asilimia 80 kwa wanawake) kwa benki shiriki kama njia ya kuongeza dhamana ya kutosha ili kuwezesha wateja kupata mikopo,”amesema Bi.Shanalingigwa
Bi.Shanalingigwa amesema ili kutimiza wajibu huo na kuwafikia watanzania wengi PASS inafanya kazi Benki 14 nchini ambazo wameingia nazo mikataba.
“PASS pia hutoa huduma za ukuaji wa biashara kama vile mafunzo mbalimbali ya wajasiriamali,upembuzi yakinifu wa miradi husika,husaidia wateja katika kuandaa maandiko ya miradi bora ya uwekezaji na kuwezesha upatikanaji wa huduma za fedha kwa ajili ya kuwezesha uwekezaji katika miradi hiyo,”amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri ameishukuru Taasisi ya PASS kwa kufanyia maadhimisho hayo Wilayani Dodoma huku akiipongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kusaidia sehemu ya mitaji,pamoja na katika masuala ya ufuatiliaji.
“Niwashukuru Pass kwa kuichagua Dodoma kufanya maadhimisho haya katika namna hiyo tunawapongeza sana kwa kazi kubwa nzuri mnayoifanya ya kusaidia sehemu ya mitaji lakini na kujenga uwezo kwa wakulima na masuala mbalimbali ya ufuatiliaji.”amesema.
Amesema hicho wanachofanya kinaendana na ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) cha kuwaondoa wakulima katika jembe la mkono na ufugaji wa kiholela na kwenda katika kilimo cha kisasa.
“Niwapongeze kwa namna ya kipekee kwa kuhamasisha yapo mambo ukiyasikia lazima akili ichangamke haraka mimi nimefarijika sana na natamani wakazi wa Dodoma message hii muizingatie,”amesema Shekimweri
Shekimweri amewataka wakulima na wafugaji kuchangamkia fursa hiyo kwani dhamana ni mali husika.
“Hakuna dhamana ya mkopo yaani tumezoea tukienda katika taasisi zingine za kifedha unaambiwa uweke dhamana ya jengo au mali fulani ya shamba kwenye ukopeshaji mdogomdogo mpaka dhamani za nyumbani, Runinga makochi unaweka kama dhamana
“Sasa unaposikia mtu anakwambia unakuja kukopeshwa madhalani Trekta au Powertiller halafu thamana ya mkopo huo ni Powertiller yenyewe sijui kama nimeeleweka yaani kuna kitu ukikisikia lazima mwili usisimke hivi na kama kweli una hamu ya kuongeza tija kwenye shughuli unazofanya hii ni muhimu sana,”amesema
Hata hivyo Shekimweri amewaomba wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Nyerere Square kuja kuona maonyesho hayo.