……………………………………………………
Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona zvyombo vya Habari vinaendelea kufanya kazi kwa uhuru lakini vizingatie Sheria zilizopo nchini.
Ameyasema hayo leo Julai 20, 2021 wakati akizungumza mubashara kwenye kipindi cha Clouds 360 kilichorushwa Kituo cha Televisheni cha Clouds.
“Matarajio yangu ni kwamba vyombo vya habari vitazingatia Sheria hii na nimeshakutana na wadau mbalimbali wa habari juu ya utekelezaji wa Sheria hii na Mhe. Rais ameshatoa maelekezo kuwa wale waliomaliza adhabu zao wapewe leseni waendelee na kazi zao”, alisema Msigwa na kuongeza kuwa tayari Idara ya Habari inakamilisha taratibu za Kidheria ili Vyombo hivyo vianze tena kufanya kazi.
Amesema wakati wa kipindi chake kama Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali vyombo vya habari vifanye kazi kwa bidii na vijivunie kuelezea maendeleo ya nchi yao.
“Ni lazima sisi waandishi wa habari pamoja na majukumu yetu na taratibu zetu za kitaaluma tuna wajibu wa kimsingi wa sisi kama watanzania kuitanguliza nchi yetu mbele”, amesisitiza Msigwa.
Kwa upande mwingine amesema kuwa kuna mchakato unaendelea ndani ya Serikali kuhakikisha eneo la kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya masuala ya habari na mawasiliano linarahisishwa ili vijana wengi waweze kujiajiri na kufanya mambo yao huko.