Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Adam Malima (katikati) na Katibu Tawala wa Mkoa huo Pili Hassan katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kabla ya kuanza ziara ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika ndani ya Mkoa huo
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) alipotembelea na kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano Horohoro Wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga. Anayefuata ni Kanali Maulid Surumbu Mkuu wa Wilaya ya Mkinga. Wengine ni watendaji alioambatana nao
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kulia) akizungumza na watendaji wa Wilaya ya Muheza kabla ya kuanza ziara yake ya kukagua ujenzi na ubora wa miundombinu ya mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya Wilaya hiyo. Kulia ni Mbunge wa Muheza Mhe. Hamis Mwinjuma
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa tatu kulia) akizungumza katika eneo la mnara wa Tigo uliojengwa kwa mchango wa ruzuku toka Serikalini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) anayefuatia ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Basilla Mwanukuzi wengine ni watendaji aliombatana nao
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (Kushoto) akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Siriel Mchembe ofisini kwake kabla ya kuanzxa ziara ya kukagua ubora na uwezo wa miundombinu ya mawasiliano katika Wilaya hiyo
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kulia) akitoa pole kwa wafiwa na waombolezaji waliokuwa katika msiba katika Kijiji cha Magila gereza Wilayani Korogwe alipotembelea kijijini hapo kukagua ubora na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika eneo hilo, kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Basilla Mwanukuzi
………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu, TANGA
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia taasisi yake ya Tume ya TEHAMA imeanzisha programu maalum ya kuwatambua, kuwasajili na kuwaendeleza wataalam, wabunifu na wabobezi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupata takwimu ya wataalam hao na kuwatumia katika kukuza uchumi wa nchi kupitia teknolojia hiyo muhimu inayogusa takribani sekta zote za uchumi, biashara na viwanda
Akizungumza katika ziara yake katika Mkoa wa Tanga aliyoifanya kwa siku mbili ya kutembelea na kukagua miundombinu ya mawasiliano na upatikanaji wa mawasiliano ya simu ya sauti na data na mawasiliano ya redio katika Wilaya ya Mkinga, Muheza, Korogwe na Handeni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ametumia fursa hiyo kuzungumza na viongozi wa Wilaya na Halmashauri kuhakikisha wataalam wa TEHAMA katika halmashauri zao wamesajiliwa na Tume ya TEHAMA
Aliongeza kuwa programu hiyo imeanzishwa kwa lengo mahsusi la kupata takwimu na kuwatambua wataalam hao katika maeneo yao ya ubobezi na kitaaluma ambapo kabla ya usajili Tume hiyo itawapa mtihani wa kufanya na atakayefuzu ndio atakayetambuliwa na kupatiwa usajili
Amesema kuwa kama Afisa TEHAMA katika Halmashauri atakuwa hana uwezo wa kumsaidia Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi katika kutatua changamoto za TEHAMA na kushughulikia masuala ya TEHAMA inamaanisha hatoshi katika nafasi hiyo
“Kama Afisa TEHAMA hana taarifa zozote kuhusu majukumu anayotakiwa kutekeleza katika eneo lake inamaanisha kuwa hatoshi katika hiyo nafasi, kila mtu anapaswa kuitendea haki nafasi aliyopewa kwasababu viongozi hawawezi kufanya kazi zote ambazo zinatakiwa kufanywa na wataalam husika”, alizungumza Mhandisi Kundo
Ameongeza kuwa Serikali ipo katika mkakati wa kuboresha na kuendeleza matumizi ya TEHAMA nchini kwa kujenga miundombinu na kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule na hospitali za umma hivyo iwapo Afisa TEHAMA atakuwa hana taarifa sahihi katika eneo lake inaweza kusababisha kurudia kupeleka vifaa katika maeneo ambayo tayari yamekwishafikiwa
Aidha, ameelekeza Maafisa TEHAMA katika Halmashauri kuhakikisha wanaandaa taarifa za hali ya mawasiliano ndani ya Wilaya ikijumuisha na teknolojia zilizopo kwenye minara ya mawasiliano kama ni ya 2G, 3G au 4G
Wakuu wa Wilaya wa Wilaya zote alizopita, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na baadhi ya wabunge waliokuwepo majimboni walishiriki katika ziara hiyo ikiwa ni pamoja na kupokea maelekezo ya maeneo ya kuyafanyia kazi yanayohusu Sekta ya Mawasiliano
Katika ziara hiyo Mhandisi Kundo alitembelea maeneo yenye changamoto za mawasiliano ya simu na data pamoja na kukagua ujenzi, ubora na uwezo wa minara ya mawasiliano hasa iliyojengwa kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari