Ukosefu wa ajira kwa miaka mingi imekuwa moja ya changamoto kubwa katika maeneo mbalimbali nchini mijini na vijijini.Tatizo hili linaathiri maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Hata hivyo, Serikali inajitahidi kutatua tatizo hilo katika maeneo mbalimbali, kwa kushirikiana na wahisani na wadau mbalimbali mfano kampuni ya madini ya Barrick.
Wakazi wa maeneo ya vijiji mbalimbali kuzunguka mgodi wa Bulyanhulu wanasifia juhudi hizo. Kwa mfano, Clementina Felix, ni mama wa watoto wawili, mkazi wa Kijiji cha Bugarama mkoani Shinyanga anasema kwa miaka mingi yeye na wanawake wenzake wamekuwa na changamoto ya kujikwamua kiuchumi na kuishi maisha duni na tegemezi.
Lakini, anasema hivi sasa yeye na wenzake wameanza kuondokana na changamoto ya maisha duni baada ya kujiingiza katika shughuli za ujasiriamali, kilimo cha kisasa na ufugaji. Anaeleza kuwa kampuni ya madini ya Barrick, inawawezesha kufanikisha ndoto zao za kujikwamua kimaisha kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali na kufadhili shughuli zao mbalimbali.
“Tulikuwa tunateseka kwa kutojua nini cha kufanya ili kujikwamua kiuchumi kwa kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji bila ujuzi na kuishia kutopata mafanikio. Tunaishukuru Barrick kwa kuja na programu inayolenga kutuwezesha kiuchumi wakazi zaidi ya 200 wa vijiji vinavyozunguka mgodi wake”, anasema Clementina huku akitabasamu.
Berita Nyawanga, yeye ni mkazi wa kata ya Mwinguru , ambako pia Barrick inaendesha programu za kuwakwamua na sasa wananchi wanafaidi. Berita anaomba kampuni kuendelea kuwezesha wajasiriamali katika maeneo yake yote ya migodi nchini hususani Wanawake na vijana ambao wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ajira.
Meneja Mahusiano ya jamii wa Barrick katika mgodi wa Bulyanhulu ,Anthony Sebastian, anafafanua uwezeshaji wajasiriamali katika maeneo yanayozunguka mgodi ni utekelezaji wa Sera ya Barrick chini ya Mpango wa Kusaidia Jamii (CSR) kuzunguka maeneo yake ya kazi. Anasisitiza kuwa wamepania kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali, kilimo cha kisasa na ufugaji.
“Kampuni inatambua kuwa ujasiriamali, ufugaji na kilimo ni maeneo ambayo yanaweza kutoa ajira kwa wananchi wengi sambamba na kuwawezesha kujikwamua kuchumi na ndo maana imeanzisha programu ya kuwezesha waanchi kutoka kata mbalimbali zinazozunguka mgodi”, alisema.
Antony anasema ili kuhakikisha shughuli zao zinakuwa endelevu kampuni Imekuwa inafadhili mafunzo ya ujasiriamali kila wiki ambapo wanavijiji hukusanyika pamoja na kupatiwa mafunzo mbalimbali ya kuendesha shughuli zao kwa ufasaha ambayo yanayolewa na wataalamu mbalimbali.Kwa wale wafugaji pia hupatiwa pia mbolea na mbegu bora.
Aliongeza kusema kuwa mbali na kuwapatia mafunzo pia kampuni Imekuwa ikiwafadhili wajasiriamali hao kuhudhuria maonyesho mbalimbali kama Sabasaba na mengineyo ili kuonyesha bidhaa zao ,kutafuta masoko zaidi na kujifunza mbinu za biashara kutoka kwa wafanyabiashara wenzao, pia alisema kuwa wajasiriamali hao wamekuwa wakiuza bidhaa zao kwa wafanyakazi wa mgodini.
Kampuni ya Barrick pia inazo progamu madhubuti za kusaidia shughuli za elimu, afya na mazingira kwa jamii kwa lengo la kuinua maisha ya wananchi.
Antony, ametaja baadhi ya miradi ya kijamii iliyotekelezwa na kampuni ya Barrick Bulyanhulu kuwa ni ujenzi wa vyumba madarasa katika sekondari ya Bulyanhulu, ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kakola,Ujenzi wa bweni la wasichana sekondari ya Bugarama, kuwezesha kituo cha Afya cha Bugarama kununua mashine ya X-ray na kutengeneza chumba cha kuhifadhi maiti.Katika kufanikisha miradi hiyo alisema kampuni imechangia zaidi ya shilingi bilioni 1.
Alishukuru kwa ushirikiano ambao kampuni Imekuwa akipiga kutoka kwa watendaji wa Serikali wa ngazi mbalimbali na kuahidi kuwa itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza changamoto za kijamii ili kuwezesha maisha ya wananchi kuwa bora.