Na Mwandishi Wetu, Singida
MAMIA ya waumini wa dini ya Kiislamu dhehebu la Answar Sunna mkoani hapa wameadhimisha ibada ya Idd Al Adha huku ujumbe mkubwa ukiwakumbusha kutowasahau masikini.
Akiongoza ibada hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya msikiti wa Al Omary jirani na stendi kuu ya mabasi Misuna, Shekhe Yaqin Said Nkokoo alisema Mwenyezi Mungu hatazami mwili wala umaarufu wa mwanadamu bali hutazama nyoyo zilizopambwa matendo mema na ucha-Mungu.
Alisema hata mwanadamu awe na umbo zuri, sura nzuri au maarufu kwa kiwango cha juu cha kidunia haina maana yoyote kama matendo yake ni chukizo mbele ya mola wake.
“Tunapokufa kinachochukuliwa ni roho pekee na sio mwili. Hata kama ulikuwa maarufu, una cheo kikubwa au mzuri wa sura na mwili kiasi gani vyote hivyo vitafukiwa ardhini na kuliwa na wadudu,” alisema Sheikh Nkokoo.
Alisema kujizuia kutowataja watu kwa mabaya, kumcha Mungu, kuepuka kufanya maasi na kuwajali wahitaji na masikini ni wajibu kwa kila muumini wa dini ya kiislamu na ndio hasa msingi wa sunna za ibada ya Eid el Hajj.
Alisisitiza katika ibada kamilifu ya swala hiyo watu hutakiwa kuchinja mnyama kama kondoo, mbuzi au ng’ombe na kisha kuwapatia masikini, ndugu na majirani na kisha familia ili kujiongezea thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu.
Aliongeza kuwa chimbuko la sikukuu hiyo ambayo huheshimiwa kama miongoni mwa sikukuu kubwa kwa waislamu duniani kote linapaswa kuchagiza imani ya kila muumini wa dini hiyo kwa tathmini ya matendo ya moyo wake angali yu hai kwa mfano halisi wa utii wa Ibrahim kwa mola wake dhidi ya jaribio la kiimani la kutaka kumchinja mwanawe.
Sheikh Nkokoo alisema uchinjaji huo ambao hufanyika baada ya swala ya Idd ni kumbukumbu ya sadaka ya Nabii Ibrahim ambaye anatajwa kwenye Kurani kuwa alikuwa tayari kumchinja mwanawe wa pekee Ismail kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu, lakini hata hivyo, Mungu alimzuia asimchinje na akampatia mnyama kondoo amchinje badala yake.
“Sikukuu hii ambayo hupatikana katika mwezi huu wa Dhul Hijjah ni sunna iliyosisitizwa kuwa ni wajibu kwa kila aliye na uwezo, na thawabu yake ni kubwa,” alisema.