………………………………………………………………………….
Ndugu wanahabari;
Leo ningependa kuwapa tathimini ya Operesheni endelevu inayofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Mei, 2021.
Kwanza niwajulishe kwamba hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari kwani matukio ya jinai na ya usalama barabarani yanaendelea kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa
Ndugu wanahabari;
Ushwari huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na misako, operesheni na ushirikiano ambao Jeshi la Polisi linaendelea kupata kutoka kwa wananchi.
Kutokana na misako, operesheni endelevu na ushirikiano kutoka kwa wananchi Jeshi la Polisi Tanzania kwa kipindi cha miezi miwili ya Mei na Juni tumefanikiwa kukamata wahalifu waliohusika katika kutenda uhalifu wa aina mbalimbali wapatao 5429.
Ndugu wanahabari,
- Waliokamatwa kwa kujihusisha na mauaji ni 275 kati yao waliokamatwa kutokana na mauaji ya wivu wa kimapenzi ni 21 imani za ushirikina ni 23 na 231 kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujitafutia kipato kwa njia za kiuhalifu.
- Unyang’anyi wa kutumia silaha waliokamatwa ni 63.
- Unyang’anyi wa kutumia nguvu waliokamatwa ni 141.
- Silaha zilizokamatwa ni 37 ikiwa ni, bastola 04, Shortgun 03, magobore 29 na Uzigun 01.
- Kuvunja nyumba na kuiba waliokamatwa kwa kipindi cha miezi hiyo miwili ni 1265.
- Kubaka waliokamatwa ni 508.
- Kulawiti waliokamtwa ni 125.
- Waliokamatwa kwa kujihusisha na makosa ya dawa za kulevya ni 2300 ambapo Heroin kiasi cha kilo 540 kilikamatwa, Cocaine gram 104, Bhangi kilo 3304.321, mashamba ya bhangi hekari 11.75 ziliharibiwa na mirungi kilo 2233.394 zilikamatwa.
- Waliokamtwa kwa kujihusisha na utengenezaji wa pombe haramu ya moshi (gongo) na kuuza ni 398 kiasi kilichokamatwa ni lita 13612.175 na mitambo ya kutengenezea pombe hiyo ni 94.
- Waganga wapiga ramri chonganishi waliokamatwa ni 15.
Aidha waliokamatwa kulingana na ushahidi ulivyowagusa wameshafikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi linaendelea kuwasihi wananchi kuendelea kushirikiana nalo ili kupata mafanikio zaidi katika operesheni zinazoendelea ili nchi yetu iendelee kuwa ya amani na utulivu.
Ndugu wanahabari,
Nipende kuchukuwa fursa hii kuwajulisha kuwa Jeshi la Polisi katika kila mkoa na kikosi limejipanga vizuri kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inakuwa shwari wakati wa waumini wa dini ya kiislam Tanzania wakiungana na waumini wenzao duniani kusheherekea sikukuu ya Eid Al-Adha.
Tunatoa wito na karipio kali kwa wahalifu kuachana na vitendo vya kiuhalifu na pia wale wote wanaondelea kuwashawishi wananchi kujiingiza kwenye vitendo vya ukiukwaji wa sheria za nchi.
Pia watambue Watanzania tunapenda kuendelea kuwa na Amani, mshikamano na utulivu hivyo kila mmoja wetu kwa nafasi yake anatakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi kwani uhalifu siku zote haulipi na mkono wa serikali una nguvu kubwa ya kuwafikia popote pale walipojificha na kupanga kutenda uhalifu.
Aksanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
David A. Misime – SACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma, Tanzania