Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizunguzumza na waandishi habari mara baada ya kuzindua kituo cha umeme katika mgodi wa Busolwa uliopo Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza, Julai 19, 2021.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo cha umeme katika mgodi wa Busolwa uliopo Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza, Julai 19, 2021.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akiwa katika picha na viongozi mbalimbali wa Mkoa na Mgodi, mara baada ya kuzindua kituo cha umeme katika mgodi wa Busolwa uliopo Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza, Julai 19, 2021.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akiwasha taa kuashiria kuwasha kwa umeme katika mgodi wa Busolwa uliopo Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza, Julai 19, 2021.
Kikundi cha ngoma kikitoa burudani mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu wa Tatu Mzunguko wa Pili, Ngazi ya Mkoa, katika kijiji cha Isolo,Kata ya Shishani, Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza Julai 19,2021.
Miundombinu ya kituo cha Umeme kilichopo katika Mgodi wa Busolwa, Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza, kituo hicho kichozinduliwa rasmi na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Julai 19, 2021.
******************************
Hafsa Omar-Mwanza
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa wito kwa Wawekezaji wa Sekta ya Madini nchini, kuunganisha umeme kwenye migodi yao ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Dkt. Kalemani, ametoa wito huo, Julai 19,2021 wakati akifungua kituo cha Umeme kwenye mgodi wa Busolwa uliopo Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza.
Aidha, amesema utumiaji wa umeme kwenye mitambo inayotumia mafuta unaokoa takribani zaidi ya nusu ya gharama ambayo wanatumia kwenye kuendesha mitambo kwa kutumia mafuta mazito.
“Naomba nitoe wito na pia nawashauri na kuwashawishi wenye migodi, kutumia umeme kwenye migodi yenu, ili kuokoa pesa zenu za uwekezaji na mpate faida kubwa na kuendeleza mitaji yenu,”alisisitiza Dkt.Kalemani.
Amesema, lengo la Serikali ni kupeleka umeme kwenye migodi yote nchini na mpaka sasa migodi 378 tayari imeshapelekewa huduma hiyo, na kwa upande wa mwaka jana jumla ya migodi 132 ilipelekewa umeme.
Aidha, amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha shughuli za kiuchumi, hasa shughuli za uchimbaji wa madini unawekewa kipaumbele kupelekewa umeme ili waweze kufanya kazi kwa tija, kupata faida na kulipa kodi.
Akikielezea kituo hicho, amesema mradi huo umefadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa maana miuondombinu yote ya kuleta umeme imefadhiliwa na Serikali.
Pia, amesema kituo hicho kimejengwa na TANESCO wenyewe bila ya msaada wa shirika lolote, na kuwapongeza kwa kazi nzuri walioifanya ya ujenzi huo.
Dkt. Kalemani, amewatoa wasiwasi wawekezaji hao kwa kuwahakikishia kuwa, umeme upo na kutosha ambao matumizi yake kwa siku ni megawati 65 kwa Mkoa mzima na unazalisha jumla ya megawati 180 na kituo hicho kinatumia megawati 4 kwa siku.
Vilevile, amewataka TANESCO na REA kuhakikisha kuwa vijiji vyote vinavyozunguka mgodi huo navyo vinaunganishiwa na umeme ili viweze kupata huduma hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa mradi, Ibrahimu Nayopa ameishukuru Serikali kwa kutekeleza ahadi ya kupekeleka umeme mgodini humo.
Amesema, huduma hiyo ya umeme imeleta manufaa makubwa katika mgodi huo pamoja na vijiji vinavyozunguka mradi, na kukamilika kwa kituo hicho kutapunguza kiasi kikubwa gharama za uendeshaji wa mtambo.
Pia, uwepo wa kituo hicho kitaongeza ufanisi mkubwa katika utendaji kazi wa mtambo wa uchenjuwaji wa dhahabu.
Katika ziara hiyo Mkoani humo, Dkt. Kalemani pia amezindua rasmi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu wa Tatu Mzunguko wa Pili, Ngazi ya Mkoa, katika kijiji cha Isolo, Kata ya Shishani, Wilayani Magu.
Mradi huo ambao utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 42, unatawajiwa kukamilika ndani ya miezi 18.