…………………………………………………………………….
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Wananchi wa kata ya Mundindi iliyopo wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wamesema bado hawana imani juu ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa liganga na mchuchuma kwakuwa miaka mingi mradi huo umekuwa ukizungumzwa bila utekelezaji wowote hivyo wanahitaji kuona utekelezaji huo kwa vitendo.
Wakizungumza hayo mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga alipofanya ziara katika vijiji vya kata hiyo kwa lengo la kusikiliza changamoto za wananchi akiwa sambamba na viongozi wa chama cha mapinduzi, wakuu wa idara ya serikali pamoja na diwani wa kata hiyo Wise Mgina.
Wananchi hao wamedai kuwa mpaka sasa hawajui mustakabali wa fidia zao hivyo ili waweze kuamini kuwa mradi huo uko mbioni kuanza wanaiomba serikali kuwalipa fidia hizo kulingana na thamani ya ardhi ya sasa.
Joshua Mtulo ni mmoja wa wananchi hao amesema kuwa wilaya na nchi kwa ujumla imekalia utajiri mkubwa sana ambao unaweza kuinua uchumi hivyo anashangazwa kuona utekelezaji wa mradi huo umekuwa wimbo na mgumu kutekelezwa.
” Mradi huu umekuwa ukizungumzwa tu! na tumekuwa tukiimba nyimbo mashuleni juu ya liganga na mchuchuma toka nipo mdogo mpaka sasa ni mzee bado mradi huo umekuwa wimbo tu kiasi kwamba imepekea tumepoteza imani na miradi hii.
Naye Joseph Mgimba ambaye ni kijana anayeishi eneo hilo amemuomba mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuwasaidia kupata ajira pindi miradi hiyo itakapoanza sambamba na kupewa elimu ya kutumia fursa mbalimbali za kibiashara ambazo zitakuwa na tija kwao na kuwapa manufaa.
Aidha kwa upande wa diwani wa kata hiyo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa tamko juu ya utekelezaji wa mradi huo sambamba na kumpongeza mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kwa kuusemea bungeni mradi huu mara kwa mara.
Pamoja na pongezi hizo diwani Mgina ameiomba serikali kuwalipa wananchi fidia zao mapema ili waweze kufanya uwekezaji katika maeneo mengine na kupata maendeleo kwani kwa sasa wananchi hao wanashindwa kufanya chochote cha maendeleo.
Ameongeza kuwa wananchi hao wakishalipwa fidia zao anaomba viwanda vijgengwe katika maeneo hayo ya mradi ili wananchi waweze kupata ajira na kunufaika pia badala ya kuchukua chuma na kupeleka katika viwanda vilivyo nje ya wilaya yao.
Kwa upande wa mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Ludewa ambaye pia katika kipindi cha mwaka 2000-2005 alikuwa mbunge wa jimbo hilo Stanley Kolimba amesema tangu mbunge wa kwanza mpaka sasa mbunge wa kumi wamekuwa wakizungumza bungeni habari za liganga na mchuchuma tu pasipo utekelezaji wowote hivyo awamu hii inaleta matumaini kidogo.
“Mimi niliwahi kuwa mbunge na niliongelea sana liganga na mchuchuma lakini haikuzaa matunda kila aliyekuja alizungumza bila mafanikio yoyote lakini kwa mwenzetu Kamonga imekuwa tofauti kwani mfupa alioushindwa fisi mwenzetu anaelekea kuuweza”, Alisema Kolimba.
Aidha kwa upande wa mbunge huyo amewataka wananchi kuwa wavumilivu juu ya ulipwaji wa fidia hizo kwani serikali ya awamu ya sita ni sikivu na itawalipa fidia zao kulingana na thamani ya ardhi huku akiwataka vijana kujikita kupata elimu za ufundi ili waweze kuwa wanufaika wa kwanza.
Amesema kuwa atahakikisha chuo cha VETA kinakamilika mapema ili vijana waweze kupata ujuzi mbalimbali utakaowasaidia kufanya kazi katika mradi huo na endapo mradi huo utaanza kabla ya chuo hicho kukamilika ataishauri serikali kuwapeleka vijana katika vyuo vilivyopo nje ya hapo.
Pia kuhusu suala la elimu na kutumia fursa zitakazojitokeza mbunge huyo amesema tayari amekwisha ongea na wizara husika juu ya kuwaleta wataalamu ili waweze kuwapa wananchi elimu ya mradi huo ambapo kwa upande wake tayari elimu ya fursa za kibiashara imeshaanza kutolewa kupitia mtaalam wa masuala ya uchumi ambaye ameletwa kwa gharama za mbunge huyo.
“Ni lazima mradi huu uanze kunufaisha wazawa, na ndiomaana nilimleta mtaalam wa uchumi ili awafundishe fursa mbalimbali za kibiashara ambazo zinaendana na wakati wa sasa ili muweze kuzitumia vyema badala ya wageni kuja kuzitumia na sisi tukizitizama”, Alisema Kamonga.