Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Mwanasha Tumbo akiwa katika ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kutembelea baadhi ya viwanda mbali mbali ikiwemo vya kutengenezea juice ya maembe cha Sayona kilichopo maeneo ya Mboga Chalizne pamoja na kiwanda cha Elven Agri kilichopo katika eneo la Mapinga Wilayani Bagamoyo.
Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani Mwanasha Tumbo wa kati kati aliyeinamisha kichwa akiwa anaangalia moja ya mitambo ambayo inatumika kwa ajili ya kuchakata zao la maembe ili kuweza kutengeneza uzalishaji wa juice.
Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani Mwanasha Tumbo wa kati kati akiwa anafafanua jambo wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kujionea shughuli mbali mbali za uzalishaji zinazofanywa na baadhi ya viwanda vya kutengenezea juice.(PICHA NA VICTOR MASANGU)
………………………………………………………………………………….
NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO
SERIKALI mkoani Pwani imesema kwamba katika kukuza sekta ya kilimo hapa nchini itahakikisha kwamba inaweka mikakati madhubuti ya kuwasaidia wakulima wa matunda kupata soko la uhakika kwa kuongeza jitihada katika kuobresha zaidi sekta ya viwanda pamoja na kuwa na miundombinu mizuri ambayo itasaidia katika upatikanaji wa malighafi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Mwanasha Tumbo wakati wa ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kutembelea baadhi ya viwanda mbali mbali ikiwemo vya kutengenezea juice ya maembe cha Sayona kilichopo maeneo ya Mboga Chalizne pamoja na kiwanda cha Elven Agri kilichopo katika eneo la Mapinga Wilayani Bagamoyo.
Katika ziara hiyo Katibu Tawala ambaye aliongozana na viongozi mbali mbali wa Mkoa wa Pwani pamoja na viongozi ngazi ya Wilaya ya Bagamoyo pamoja na wataalamu mbali mbali wa kilimo lengo ikiwa ni kujoene shughuli mbali mbali za uzalishaji mali na bidhaa amabzo zinazalishwa katika viwanda hivyo pamoja na kubaini changamoto zilizopo ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi.
“Kwa kweli nimeweza kupata fursa ya kutembelea baadhi ya viwanda vilivyopo katika Wilaya yetu ya Bgamoyo lakini kitu kikubwa ambacho kwa upande wangu nimeweza kukibaini katika kiwanda hiki cha Sayona kwa sasa wanazalisha chini ya kiwango maana wanatakiwa kuzalisha tani zipatazo 180 lakini kwa sasa wanajikuta wanazalisha tani 18 tu kwa hiyo sisi ndio maana tumepita ili kujionea hali halisi lengo letu ni kushirikiana kwa pamoja ili tuweze kuona namna ya kuwasaidia wawekezaji wetu,”alisema.
Pia alibainisha kwamba lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuendelea kushirikiana bega kwa bega na wawekezaji wa viwanda mbali mbali kwa nia ya kuwasikiliza changamoto zao walizonazo ili kuweza kuwasaidia kwa hali na mali katika suala zima la kutimiza malengo ambayo wamejiwekea ikiwemo kutoa fursa za ajira sambamba na kukuza uchumi wa nchi.
“Katika viwanda hivi vyote viwili kwa sasa vinahitaji zao la embe ili kuweza kuongeza kasi zaidi ya uzalishaji kwa hivyo katika Mkoa wetu wa Pwani kunahitajika zaidi upatikanaji wa maembe kwa wingi ambayo yataweza kuvisaidia viwanda hivyo kuweza kuongeza kasi ya uzalishaji wa tani nyingi zaidi tofauti ya kwa sasa ilivyokuwa uzalishaji bado upo katika kiwango cha chini,”alifafanua Katibu Tawala huyo.
Kadhalika katika hatua nyingine alitoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Pwani pamoja na wakulima kuhakikisha wanaongeza kasi zaidi ya kulima zao la maembe ya aina mbali mbali kwani fursa ya uhakika kwa ajili ya kupata soko upo mkubwa hivyo wanapaswa kushirikiana na wataalamu wa kilimo kwa ajili ya kupata maelekezo mbali mbali katika kulima kilimo chenye tija.
Aliongeza kuwa uwepo wa wawekezaji mbali mbali hasa katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata matunda ndio dhumuni kubwa la serikali ya awamu ya sita ili kuweza kufungua fursa mbali mbali za ajira katika makundi mbali mbali na kuweza kuwakwamua wananchi kiuchumi pamoja na kuondokana na wimbi la umasikini.
Katibu huyo katika kutimiza azma ya serikali aliwataka wataalamu wa kilimo kuweka mipango madhubuti ya kuwafikia wakulima katika maeneo mbali mbali ili kuwapa elimu zaidi juu ya kilimo cha zao la maembe ikiwa sambamba na kuongeza zaidi juu ya mkazo katika kufanya utafiti katika zao hilo la maembe ambayo yanahitajika na viwanda husika.