Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( kwanza-kushoto) akizungumza na wananchi wa kisiwa cha Maisome, kilichopo Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza, wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa mradi wa umeme wa jua unaotekelezwa katika kisiwa hicho
Wananchi wa kisiwa cha Maisome, kilichopo Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(hayupo pichani) wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa mradi umeme wa jua unaotekelezwa katika kisiwa cha Maisome, kilichopo Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na mwenyekiti wa kijiji cha Kanoni, wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa mradi umeme wa jua unaotekelezwa katika kisiwa cha Maisome, kilichopo Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza
Miundombini inayotumiwa kuzalisha umeme wa jua na Kampuni ya JUMEME iliyopo katika kisiwa cha Maisome, kilichopo Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza
…………………………………………………………………………………………
Hafsa Omar- Mwanza
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka umeme wa gridi ya Taifa katika kisiwa cha Maisome, kilichopo Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza.
Agizo hilo amelitoa, wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa mradi umeme wa jua unaotekelezwa katika kisiwa hicho.
Akizungumza na wananchi, amesema kuwa suluhisho la kudumu la kutatua tatizo la umeme katika kisiwa hicho ni kuunganishwa na gridi ya Taifa.
“TANESCO na REA nataka mkajipange ndani ya miezi mitatu mlete umeme wa gridi huku ,Serikali inawaletea umeme wa kudumu wa gridi ya Taifa ambao utasaidia kuondoa hizi changamoto zote,”alisema
Aidha, amesema Serikali itahakikisha kuwa Watanzania wote wanapata umeme wa uhakika na wa bei nafuu kwa wakati wote.
Amesema, Serikali imetoa jumla shilingi bilioni 5.2 kwaajili ya kuleta umeme wa jua ( Solar) kwenye eneo hilo ili wananchi wapate huduma hiyo.
Dkt. Kalemani ametoa agizo kwa kampuni inayosambaza umeme katika kisiwa hicho JUMEME kuwauzia umeme wananchi kwa bei ya unit moja kwa shilingi 100 ili wananchi hao wapate umeme wa bei nafuu.
“walikuwa wanauza umeme kwa unit moja shilingi 3700, 3500 wakaja 2500 lakini kuanzia Alhamisi bei ya umeme huku siku zote itakuwa ni shilingi 100 kwa unit , Mhe Rais anataka watanzani wote wapate umeme tena umeme wa bei nafuu,” alisema.
Alifafanua kuwa, Serikali mwaka juzi iliwaita wazalishaji wote wa umeme nchini na kuwaelekeza kuuza umeme kwa bei elekezi ambayo haitawaumiza Watanzania.
Pia, amewataka wasambazaji hao kutoa huduma hiyo kwa masaa ishirini na nne bila ya kuwaekea mgao au kukatika bila ya sababu maalumu, kwakuwa wananchi hao wanahitaji huduma hiyo kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Vilevile, amewagiza wasambazaji hao kufungua ofisi katika eneo hilo ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi na kwa wakati wote na kuwataka kuendelea kusambaza umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobaki.
Nae, Mbunge wa jimbo la Buchosa, Erick Shigongo, amemshukuru Waziri wa Nishati, kwa kazi nzuri anayofanya ya usimamizi wa usambazaji wa umeme na kwa kutatoa mzozo wa bei umeme katika kisiwa hicho.
Pia, amewataka wananchi wa kisiwa hicho kuendelea kutumia huduma hiyo kwa shughuli mbalimbali za kuichumi.