KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Shaka Hamdu Shaka,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 19,2021 jijini Dodoma wakati akitoa tathimini ya uchaguzi uliofanyika jimbo la Konde Wilaya ya Micheweni Kaskazini Pemba
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Shaka Hamdu Shaka,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo Julai 19,2021 jijini Dodoma wakati akitoa tathimini ya uchaguzi uliofanyika jimbo la Konde Wilaya ya Micheweni Kaskazini Pemba .
……………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuona haja ya kuangalia namna ya kufanya mapitio upya ya Sera na sheria za kodi ili kuliweka vyema suala la tozo na miamala ya simu ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 19,2021 Jijini Dodoma na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Shaka Hamdu Shaka wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa Rais Samia amedhihirisha hekima, usikivu wake, uzalendo, umakini katika utendaji wake.
Hatua hiyo imekuja baada ya uamuzi wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wa kutaka tozo za miamala ya simu kuangaliwa upya na kuweka unafuu kwa wananchi.
”Mama amedhihirisha kwa namna ambavyo amekuwa akiguswa moja kwa moja na changamoto za Watanzania na haki hii ni kielelezo tosha kuwa huyu ni Rais wa watu lakini na nao watu wanarais wao ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan,”amesema Shaka
Pia amezitaka Serikali ya Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia kuona namna gani zitafanya mapitio ya sera, sheria za kodi ili kuliweka vyema jambo hili katika utekelezaji wake.
“Serikali zote mbili ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zote zinatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2020-25, CCM inaelekeza serikali kupitia Ilani hii ya uchaguzi wakati ikitekeleza maelekezo ya Rais ya kupitia upya, chama kinaagiza serikali ziangalie namna ya kufanya mapitio ya sera na sheria za kodi.”amesema Shaka
Amesema kuwa Chama hicho kipo imara na kinaendelea kujipambanua na ndio maana waliposikia na kuona jambo hili likiendelea katika mitandao ya kijamii wao kama chama wakaona si suala la kulifumbia macho.
Hata hivyo Shaka ametoa tathimini ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo la Konde na kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kukipatia ushindi Chama cha Mapinduzi CCM.
Amesema kuwa Sheha Faki kutoka CCM alipata kura 1796 na Mohamed Issa wa ACT wazalendo alipata kura 1373 ,Mohamed Said wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA alipata kura 857 na Salama Omary wa Chama cha Wananchi CUF alipata kura 624.
“Kwa niaba ya chama niwahakikishie kuwa hawatajuta juu ya uamuzi wao wa kukipa ushindi chama cha Mapinduzi, wamekikopesha chama Imani na tutalipa Imani katika kuwaletea maendeleo endelevu,”amesema.
Aidha amesema kuwa chama kimekuwa mstari wa mbele katika kuwasimamia viongozi katika ngazi zote ili kuhakikisha kuwa wanatimiza dhamira na matakwa ya wananchi katika kuwaletea maendeleo.