*************************
Na Lucas Raphael,Tabora
Katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya mama lishe na madereva wa malori ya mizigo wanaotumia stendi ya maegesho ya malori iliyoko wilayani Igunga mkoani Tabora wanalazimika kujisaidia haja ndogo na kubwa katika vibanda vya biashara vilivyoko kwenye maegesho ya stendi hiyo ambavyo havijakamilika.
Wakizungumza kwa masikitiko kwenye eneo la standi baadhi ya madereva wa malori ya mizigo yanayofanya safari zake ndani ya nchi na nje ya nchini ikiwemo Burundi, Rwanda baadhi ya madereva hao Mrisho Juma, Abdallah Said, Kibadeni Ramadhani na Samson Jackson wamesema stendi ya maegesho Igunga inakabiliwa na upungufu wa miundombinu ya matundu ya vyoo ambapo hivi sasa kuna matundu mawili tu ya akinamama ambayo wanachangia pamoja na wanaume huku kukiwa na mlango mmoja wa kuingilia.
Kibadeni alibainisha kuwa pamoja na wao kulipa ushuru wa kuoga Sh. 500 kujisaidia haja ndogo na kubwa sh. 300 pamoja na kuegesha lori hapo wamekuwa wakilipa sh. 3000 lakini halmashauri imeshindwa kuboresha miundombinu ya matundu ya vyoo kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu.
Hata hivyo Mrisho Juma alisema kutokana na hali hiyo kumekuwa na msongamano mkubwa wa kusubiriana hali ambayo imekuwa ikilazimika baadhi ya madereva na wananchi wanaotumia maegesho hayo wamekuwa wakilazimika kujisaidia kwenye vibanda vilivyowazi ambavyo vimejengwa na wafanyabiashara na kushindwa kuviendeleza ambapo vichaka vimeshamiri.
Aidha Samsoni Jackson aliongeza kuwa ni jambo la aibu kuona wanawake na wanaume wakitumia mlango mmoja kuingia wanapojisaidia na kuiomba serikali ya wilaya kupitia mkuu wa wilaya hiyo waangalie eneo hilo kwa jicho la huruma.
Nae mmoja wa mama lishe Anna Simon akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema kitendo cha kuchangia choo na wanaume ni jambo la aibu ambapo alisema kumekuwa kukisababisha baadhi ya akinamama kwenda kujisaidia kwenye vibanda na kuomba serikali kuchukua hatua za haraka kwa kuwa nzi wanaotoka kwenye vinyesi hivyo wamekuwa wakitua kwenye vyakula vyao jambo ambalo linaloweza kuleta mlipuko wa magonjwa.
Nae mmoja wa waziba pancha katika maegesho hayo Moka Changalawe alisema maegesho hayo yana changamoto nyingi ikiwemo kutokuwa na miundombinu mizuri ya maegesho ambapo nyakati za masika maji yamekuwa yakituama katika eneo hilo.
Sanjari na hayo Changalawe alisema kutoendelezwa vibanda na wafanyabiashara kumesababisha kuota msitu ndani ya vibanda hivyo ambapo baadhi ya vibaka wamekuwa wakijibanza humo huku wengine wakijisaidia katika maeneo hayo na kuiomba halmashauri kuboresha vibanda hivyo hali itakayosaidia halmashauri kupata mapato ya kutosha.
Nae mtoza ushuru katika maegesho ya malori Alfred Kasimili alisema kuna matundu manne ya vyoo ambapo mawili ya wanawake na mengine mawili ya wanaume sambamba na bafu na kusema kuwa hivi sasa matundu yanayotumika ni mawili ambapo wanachangia wanaume na wanawake huku mlango wa kuingia ukiwa mmoja.
Kasimili alifafanua kuwa egesho hilo la malori linalaza malori kwa siku 70 hadi 80 na kila lori moja ushuru wake ni sh. 3000 huku ushuru wa kuoga sh. 500 na kujisaidia sh. 300.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Pascrates Kweyamba alipoulizwa juu ya changamoto hizo alikiri kuwepo “ni kweli hivi karibu kuna mwananchi mmoja anayeitwa Moka Changalawe alinipigia simu akiomba tufike eneo hilo na kweli tulikwenda tukaziona changamoto hizo na hivi sasa tunakarabati matundu mengine ya vyoo hivyo tunaomba wanaotumia eneo hilo wawe na Subira.
Hata hivyo kaimu mkurugenzi huyo aliongeza kuwa halmashauri imejipanga kuboresha kikamilifu katika eneo hilo sambamba na maeneo ya stendi mengineyo kwa mwaka huu wa fedha.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Lucas Bugota alisema kamati ya fedha na mipango ilishatembelea eneo hilo la maegesho na kulalamikiwa na baadhi ya wananchi kuhusu suala la vyoo ambapo walimuagiza mkurugenzi ndani ya wiki mbili vyoo viwe vimekarabatiwa vyote lakini ameshangazwa kuona hadi sasa ukarabati bado haujakamilika na kusema kuwa atafuatilia kwa haraka suala hilo.