Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akizindua kituo cha afya cha Nyaruyoba kilichopo kata ya nyaruyoba wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma. Julai 17 , 2021
Kituo hicho kinahudumia wakazi Zaidi ya elfu 19 wa eneo hilo na maeneo jirani. Baada ya uzinduzi huo Makamu wa Rais akazungumza na wananchi wa eneo hilo.
*******************
Makamu wa Rais ameendelea na ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Kigoma. Katika siku ya tatu ya ziara yake, Makamu wa Rais ametembelea wilaya za Kasulu pamoja na Kibondo.
Akiwa njiani kuelekea wilayani Kibondo, Makamu wa Rais amesimama katika maeneo mbalimbali kuwasalimia wananchi waliojitokeza kumlaki mkoani humo. Akiwa katika eneo la nyakitonto wilayani Kasulu , Makamu wa Rais amepokea malalamiko ya wananchi kusumbuliwa mna kupigwa na askari wa uhifadhi kwa madai ya kuingia katika eneo la pori la kagerankanda ambalo wananchi wanadai ni eneo wanalotumia kwa shughuli za kiuchumi. Ameagiza kupatikana kwa ufumbuzi wa haraka wa mipaka ya pori la Kagerankanda ili kuepusha migongano kati ya wananchi na idara ya maliasili na utalii wilayani humo. Makamu wa Rais ametoa onyo kwa askari hao kuacha kujichukulia sharia mkononi kwa kuwaadhibu wananchi badala yake watumie vyombo husika katika kutatua migogoro yao.
Akiwa katika Kijiji cha Makere, Makamu wa Rais amewahakikishia wananchi wa eneo hilo kwamba nia ya serikali ni kuunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa mingine kwa barabara za lami hivyo wananchi wa Makere kunufaika na barabara hizo. Kuwepo wa changamoto ya maji katika Kijiji hicho , waziri wa maji Jumaa Aweso amesema licha uwepo wa mradi wa kisima cha lita elfu 45 kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ( Water Mission) kijijini hapo lakini pia wizara inatarajia kuchimba kisima kingine ili kutosheleza huduma ya maji katika eneo hilo.
Akiwasalimu wananchi katika eneo Busunzu wilaya ya Kibondo, Makamu wa Rais amesema miradi ya kijamii inayoambatana na ujenzi wa barabara inayopita katika eneo hilo itatekelezwa kama ilivyopangwa ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya, ununuzi wa gari la kubebea wagonjwa, kujenga shule ya msingi pamoja na kujenga miundombinu ya maji.
Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais amezindua kituo cha afya Nyaruyoba kilichopo Kibondo mkoani Kigoma. Kituo hicho kinahudumia Zaidi ya wananchi elfu 19 kutoka katika kata ya Nyaruyoba na maeneo ya jirani. Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Nyaruyoba kwani hapo awali ndio walioibua mradi huo na baadae kuongezewa nguvu na serikali hadi kufikia kuwa kituo cha afya.
Aidha Makamu wa Rais amewasisitiza wananchi wa eneo hilo kuendelea kuchukua tahadhari zote dhidi ya ugonjwa wa Korona. Amewaagiza viongozi wa serikali kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo kwani mkoa wa Kigoma unatajwa kuwa kati ya mikoa kumi inayoongoza kwa maambukizi nchini.