Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA)
umevunja rekodi ya kusajili na kutoa
vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi takribani 10,495 ndani ya siku 16 katika
Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama SabaSaba.
Akitoa taarifa hiyo kutoka katika banda la RITA
viwanja vya SabaSaba, Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (RITA), Emmy Hudson amesema kuwa safari hii wananchi wengi
wameonesha kuwa na muitikio mkubwa wa kufuatilia vyeti vya kuzaliwa na hii ni
kutokana na kujua umuhimu wa kuwa na cheti hicho ili kujipatia mahitaji muhimu
katika jamii yetu.
Aidha, wananchi wameipongeza RITA kwa huduma ambayo
wameitoa katika maonesho hayo bila ubaguzi wowote na bila usumbufu ambapo kila
aliyehitaji huduma ya cheti cha kuzaliwa alipewa.
Hudson amesema hayo mkoani Dar es Salaam wakati
akizungumza na wananchi waliofika katika banda la RITA kwa ajili ya kupata
vyeti vya kuzaliwa siku ya kufungwa kwa maonesho hayo, ambapo yalifungwa rasmi na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
Amesema hatua hiyo, ni sehemu ya mkakati wa RITA
kuwafikia wananchi katika kila sehemu na kutoa huduma pamoja na kwenye
maadhimisho na maonesho mbalimbali kama hayo ili kuwarahisishia upatikanaji
wake karibu na maeneo wanayoishi.
Hudson amesema licha ya maonesho hayo kumalizika bado
wataendelea kutoa huduma hiyo katika ofisi za RITA kama kawaida hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kufika
katika ofis za RITA ili kupata vyeti vya kuzaliwa kwani ni haki ya kila
mtanzania kuwa na cheti hicho.
Pia, amesema RITA iko imara kwa kutoa huduma hiyo,
kwasababu changamoto waliyoipata katika maonesho hayo ni watu kuwa wengi ambapo
hatahivyo waliweza kuhakikisha kuwa kila aliyefika katika banda la RITA alipata
huduma stahiki.
“Changamoto tuliyoipata ni watu kuwa wengi,
ambapo ikasababisha huduma hiyo kutolewa hadi saa moja usiku, ili kila
aliyefika katika banda hili aweze kupata huduma kulingana na mahitaji
yake,” Alisema Bi. Hudson.
Mmoja wa wananchi hao aliyejulikana kwa jina la
Bi.Amina Abdallah ameipongeza RITA kwa huduma ambayo wameitoa na yeye kuweza
kufanikiwa kupata cheti chake cha kuzaliwa kwa gharama nafuu na kwa haraka.
Amesema “kwakweli wananchi tulikuwa wengi sana
ambao tunahitaji huduma ya vyeti, lakini tulipokelewa vizuri na maafisa wa
RITA waliokuwa wanatoa huduma na
kutuhudumia kulingana na mahitaji yetu,naipongeza sana RITA kwa kutuletea
huduma hii kwenye maonesho haya makubwa”
Naye, Bwana Joseph Mashaka amesema kuwa, hakuwahi
kutegemea kupata cheti cha kuzaliwa kulingana na umri wake kutokana na baadhi
ya wananchi huko mtaani kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu ugumu wa kupata huduma hiyo, lakini mara baada ya
kufika katika banda hilo alipewa maelekezo na kisha kuanza hatua za kupata
cheti tofauti na alivyodhani hapo awali.
“Tunashukuru kupata huduma hii hapa hapa
sabasaba, Mimi ni mkazi wa Chanika kwangu ilikuwa rahisi kufika hapa kwa sababu
kila nilipotamani kuifuata huduma hii katika ofisi zao nilikuwa naona uvivu kwa
kuona kuwa ni mbali,” amesema Mashaka
Mmoja wa viongozi waliotembelea banda hilo ni Meya wa
Jiji la Ilala, Mhe. Omary Kumbilamoto ambapo aliupongeza Wakala kwa kutoa
huduma hiyo hadi muda wa usiku kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anapata
huduma ya cheti cha kuzaliwa.
“Kazi nzuri sana mnafanya, mmejitolea kufanya
kazi hadi usiku ili wananchi waweze kupata vyeti vyao kwa kufuata utaratibu,
msiishie hapa tu endeleeni kupeleka huduma hii karibu na jamii,” amesema
Kumbilamoto.
Maonesho hayo ya 45 ya Kimataifa ya Biashara
yajulikanayo kama SabaSaba yalifungwa rasmi tarehe 13 Julai ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa pili
wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla.
Kaimu Kabidhi
Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Emmy Hudson
akizungumza na wananchi katika banda la
RITA wakati maonesho 45 ya Biashara ya Kimataifa ya
Sabasaba yaliyofanyika mwezi huu kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara
ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Afisa Mawasiliano wa
(RITA) Jafari Malema (kushoto) akizungumza na wananchi na waliofika kwenye banda la RITA katika
maonesho 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yaliyofanyika mwezi huu kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es
Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka Michuzi TV) kushoto Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA),Emmy Hudson.
Msajili Mwandamizi kutoka
RITA, Rehema Mushi wakwanza kulia akiwa pamoja na maafiza wenzake wakiwahudumia wananchi waliofika kwenye banda
la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) katika maonesho 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yaliyofanyika mwezi huu kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es
Salaam.