MKUU wa Mkoa wa Dodoma Athony Mtaka,akizungumza na wanafunzi wakati wa ziara ya kukagua na kujionea maendeleo ya elimu katika shule ya Msingi Michese iliyopo Kata ya Mkonze Jijini Dodoma ambapo aliongozana na Mkuu wa wilaya ya Dodoma mjini,Mbunge wa Jimbo la Dodoma pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa.
Mkuu wa wilaya ya Dodoma mjini Jabir Shekimweri,akizungumza na wanafunzi wa shule ya Msingi Michese iliyopo Kata ya Mkonze Jijini Dodoma
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Msingi Michese iliyopo Kata ya Mkonze Jijini Dodoma wakiwa darasani na mwalimu wao.
Muonekano wa madarasa ya shule ya Msingi Michese iliyopo Kata ya Mkonze Jijini Dodoma
………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Athony Mtaka amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Joseph Mafuru kushughulikia changamoto ya uhaba wa vyumba vya Madarasa katika shule ya Msingi Michese.
Agizo hilo amelitoa mara baada ya kufanya ziara ya kukagua na kujionea maendeleo ya elimu katika shule hiyo iliyopo Kata ya Mkonze Jijini Dodoma huku akiongoza na mkuu wa wilaya ya Dodoma mjini,Mbunge wa Jimbo la Dodoma pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa.
”Nakuomba Mkurugenzi wa jiji ushughulikia changamoto hiyo ya Uhaba wa vyumba vya madarasa kwani tayari Serikali ilishapitisha bajeti ya elimu hivyo katika fedha watakazo pokea wahakikishe wanaifikia shule hiyo ya Michese.
“Ili kuwe na ufaulu mzuri lazima miundombinu ya elimu iwe mizuri hasa ukizingatia kumekuwa na ugonjwa wa covid 19 na wanafunzi wengine kukaa chini kwa ukosefu wa madawati hii kwetu ni aibu”amesema Mtaka.
Pia Mtaka ameelezea kuwa shule hiyo kuwa katikati ya jiji la Dodoma bado haina hadhi hivyo wahusika nawaomba mfanye ukarabati wa miundombinu ya majengo na Nyumba za walimu ikiwemo ujenzi wa vyoo vya walimu na huduma za maji shuleni hapo.
“Katika Karne hii kweli bado kuna shule ambazo wanafunzi wanakaa chini ,!?lazima sisi kama viongozi tuzitendee haki nafasi zetu Katika kutoa huduma hasa katika masuala ya Elimu ili Watoto wetu wasome kwa ari,”ameongeza Mtaka
Hata hivyo amewataka wazazi kuacha kuwapa watoto majukumu mengi ya kazi za nyumbani na badala yake kuwaachia muda mrefu wakiwa nyumbani wapate muda mwingi wa kujisomea kwakuwa elimu ndio msingi wa maisha yao.
“Hapa Kuna baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwatumikisha watoto kufanya kazi za nyumbani Kama kuosha vyombo, kufua,kuchota maji na kuwafanya watoto kuchoka ,wanashindwa kupata muda wa kujisomea hasa wenye watoto wa madarasa ya mitihani Kama darasa la nne na la Saba hakikisheni mnawapunguzia watoto majukumu ya kazi “amesisitiza
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini Jabir Shekimweri amesema kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa vilivyopo atachangia mifuko mia moja ya saruji ili waweze kufyatua matofali waweze kuanzisha ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.
Awali akitoa taarifa Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Michese Mwalimu Sizya Wiliam amesema shule hiyo inajumla ya wanafunzi 1850, vyumba vya madarasa tisa na inaupungufu wa madawati 100 .
Pia amesema kuwa shule hiyo bado inakabiliwa na Uhaba wa vyoo vya walimu ambapo kwa sasa wanajisaidia kwa kuchanganyika kwa kutumia vyoo vya wanafunzi na kwa majirani na shule hiyo.
“Ni jambo la aibu kwetu ,shule yetu inakabiliwa na changamoto nyingi kama unavyoona ,mkundikano katika vyumba vya madarasa na pia tuna uhaba wa madawati hata hivi vyumba vya madarasa tisa vilivyopo ni chakavu kabisa”amesema
Aidha ameeleza kuwa shule hiyo ina uhaba wa walimu kwani ina walimu 30 na kati yao mmoja ni wakujitolea hivyo walimu waliopo hawaendani na idadi ya wanafunzi waliopo jambo linapelekea kushuka kwa ufaulu shuleni hapa.