MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka,akizungumza na wananchi wa eneo la Michese Kata ya Mkonze jijini Dodoma kwenye ziara yake ya kusikiliza migogoro ya ardhi kwa wananchi.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka,akisisitiza jambo kwa wananchi wa eneo la Michese Kata ya Mkonze jijini Dodoma kwenye ziara yake ya kusikiliza migogoro ya ardhi kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ,Jabir Shekimweri,akizungumza na wananchi wa eneo la Michese Kata ya Mkonze jijini Dodoma wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka ya kusikiliza migogoro ya ardhi kwa wananchi.
Baadhi ya wananchi wakielezea kero zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka.
Baadhi ya wakazi wa Michese wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka,(hayupo pichani) wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Michese Kata ya Mkonze jijini Dodoma kwenye ziara yake ya kusikiliza migogoro ya ardhi kwa wananchi.
………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka ameisimamisha kazi Kampuni ya upimaji Ardhi ya Geoplanea Ltd,kutokana na kulalamikiwa na wananchi wa eneo la Michese Kata ya Mkonze kuilalamikia kwa madai ya kuwadhulumu maeneo yao na kuyauza.
Pia ameagiza kazi ya upimaji ifanywe na Wataalam wa Jiji la Dodoma pamoja na Wizara ya Ardhi,Nyumba na maendeleo ya makazi.
Kauli hiyo aliitoa wakati akisikiliza kero za wananchi wa eneo la Michese Kata ya Mkonze jijini Dodoma kwenye ziara yake ya kutokomeza migogoro ya ardhi kwa wananchi kampeni ijulikanayo kwa ziro migogoro ya aridhi Dodoma mkuu huyo amesema kampuni hiyo inasimamishwa kwa kukiuka masharti ya utendaji kazi wake.
“Viongozi wote kwa pamoja tumejadili na tumeamua kuanzia sasa kampuni hii ya Geoplan tunaisimamisha kufanya kazi na hivyo basi shughuli zote za upimaji zitafanywa na jiji kwa kushirikiana na wizara ya ardhi,”amesema Mtaka.
Aidha Mtaka amewataka wananchi hao wa Michese kutouza maeneo yao yaliopimwa ili wasilete migogoro mingine na hao walio wauzia.
”Wananchi nawaomba mheshimu maeneo yaliyopimwa kutofanya chochote hadi hapo uongozi wa Jiji na Wizara ya Ardhi watakapoenda tena”amesisitiza Mtaka
Hata hivyo Mtaka ametoa agizo kuwa makampuni yote yanayofanya kazi na jiji wayafuatilie na kuyachunguza kama hayana migogoro ili kulisaidia jiji kulipa fedha zisisokuwa na msingi.
“Nayasema haya kawasababu jiji limekuwa likidaiwa jumla ya shilingi Bilioni 4 na makampuni yanayojishuhulisha na upimaji wa ardhi, na hali hiyo imepelekea migogoro kuongezeka Dodoma ,”amesema Mtaka .
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri amesema kuwa asili ya mgogoro wa eneo hilo ni kutokana na upimaji na urasimishaji wa eneo na hivyo kupelekea malalamiko hayo na kuamua kuja na uongozi wa Mkoa ili kusikiliza kero za wakazi wa Michese.
Awali wakielezea kero zao baadhi ya wakazi hao wa michese wamesema kuwa wanashangazwa na kitendo cha Kampuni hiyo ambayo imekuwa ikipima maeneo hayo na kujimilikisha kinyume na taratibu.
“Mkuu wa mkoa bora umekuja najua utatusaidia kwasabu tumenyanyasika kwa muda mrefu na hii kampuni, sisi hatuitaki kwasababu imekuwa haitutendei haki licha ya kutupimia maeneo lakini imekuwa ikijimilikisha maeneo mengine”,walisema.
Wamesema kuwa licha ya wao kuwa na kamati ya usimamizi wa Kampuni hiyo katika eneo la Michese hakuna kinachofanyika zaidi ya kuchukuliwa maeneo yao jambo ambalo wamesema sio haki.