Mwezeshaji kuoka Shirika la CWCD Epiphania Josepahati akizungumza na washiriki wa mafunzo wakati wa utambulisho wa mradi wa HEBU TUYAJENGE unaolenga kuhamasisha jamii kupima VVU/UKIMWI kwa watoto na vijana
Picha ya Pamoja ya Washiriki wa mafunzo ambao ni Wataalamu kutoka Sekta mbalimbali Halmashauri ya Mji Njombe wakiwa pamoja na wawezeshaji na Katibu Tawala Wilaya Bw, Emmanuel George wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo
Washiriki wa mafunzo wakipitia vipengele mbalimbali kuhusu hati ya maridhiano itakayosainiwa na Halmashauri na KONGA (Baraza la Watu wanaoishi na Maambukizi ya VVU Katika Halmashauri) kwenye kufanikisha utekelezaji wa mradi wa HEBU TUYAJENGE
Waheshimiwa Madiwani kutoka katika Kata tano za Halmashauri ya Mji Njombe zinazoanza kutekeleza mradi wakiendelea na mafunzo
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji NJombe Mheshimiwa Erasto Mpete akipata ufafanuzi kutoka kwa mwezeshaji wa shirika la CWCD wakati wa mafunzo ya utekelezaji wa mradi wa HEBU TUYAJENGE
Wataalamu mbalimbali wa Halmashauri wakiendelea na mada
…………………………………………………………………………………..
Hyasinta Kissima-Afisa Habari
Halmashauri ya Mji Njombe
Ni mafunzo kwa Waheshimiwa Madiwani kutoka katika Kata tano za Halmashauri zitakazotekeleza mradi na Wataalamu mbalimbali yakiendeshwa na Asasi isiyo ya Kiserikali CWCD(Centre for Women and Children Development) kupitia Mradi wa HEBU TUYAJENGE ambapo mkakati wa mradi huo umelenga kuongeza idadi ya Watoto na Vijana wenye VVU na UKIMWI Katika huduma tiba na matunzo kwa njia njia ya kuboresha rufaa.
Akifungua mafunzo hayo Katibu Tawal Wilaya ya Njombe Emmanuel George amesema kuwa ili kufanikisha 95 ,95,95 kwa kupima, kujua afya na kuanza matumizi ya dawa na kwa wale wasiokutwa na maambukizi kuendelea kuihamasisha jamii kujilinda washiriki wanapaswa kuhakikisha kuwa elimu wanayoipata inafika kwa jamii.
“Niwaombe wadau ambao wengi wenu humu ni viongozi kuhakikisha kuwa tunakwenda kupunguza maambukizi kwa kwenda kutekeleza yale yote tutakayojifunza hususani kwa jamii na kwa kuzingatia uwepo wa matukio ya kikatili yaliyopo katika Wilaya ya Njombe.”Alisema Katibu Tawala
Aliendelea kusema “Licha ya kuwa kumekua na Asasi zinazojishughulisha na mapambano ya VVU/UKIMWI bado kuna kundi kubwa la Watendaji, Wenyeviti, Viongozi wa Dini ambao ni muhimu kwao kupatiwa mafunzo haya kwani hao ndio wenye Wananchi na rahisi kwao kuifikia jamii hivyo amezitaka Asasi hizo kuona ni kwa namna gani makundi hayo yanahusishwa ili lengo la kutokomeza unyanyapaa na maambukizi liweze kufanikiwa.”Alisema
Wakizungumza wakati wa kuwasilisha mada mbalimbali juu ya mradi wa Hebu Tuyajenge,Wawezeshaji kutoka Asasi ya CWCD Epiphania Josephat na All Mbwego wamesema kuwa kupitia mafunzo hayo ya kutumia gurudumu la rufaa itasaidia kufikia lengo la kuongeza idadi ya Watoto na Vijana katika tiba na matunzo.
Kwa upande wake Katibu wa KONGA Halmashauri ya Mji Njombe John Msofu amesema kuwa jambo kubwa la kipekee ambalo wanatarajia litasaidia kwenda kuleta matokeao chanya kwenye jamii ni ushirikishwaji wa WAVIU kwenye utekelezaji wa mradi huu jambo ambalo litakwenda kuleta hamasa zaidi kwa jamii. Aidha wameitaka Halmashauri kuhakisha kuwa kwa Asasi zisizo za Kiserikali zinazopenda kutekeleza miradi ya UKIMWI kuhakisha kuwa wanawashirikisha KONGA (Baraza la Watu wanaoishi na Maambukizi ya VVU Ngazi ya Halmashauri ) badala ya kwenda mojamoja kwenye jamii.
Sambamba na hilo Washiriki pia waliweza kupitia mada mbalimbali ikiwemo hati ya maridhiano kati ya Halmashauri na KONGA ili kutekeleza majukumu na wajibu wao na kwa sasa zoezi la majaribio linaendelea kwa Mawakili Tiba kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii wakiwemo Vijana na Watoto na kwa wale wenye maambukizi kuweza kuwaunganisha na huduma.
Ikumbukwe kuwa katika Halmashauri ya Mji Njombe Mradi huo utatekelezwa katika Kata tano za Halmashauri ikiwemo Njombe Mjini, Mjimwema, Makowo, Yakobi na Uwemba na utadumu kwa muda wa miaka mitano.