Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb), akiuagiza uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Zanzibar, kuhakikisha unasimamia Sheria ya Bima kwa kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini zinakatiwa Bima na Kampuni zilisosajiliwa nchini, alipotembelea TIRA Zanzibar, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo visiwani Zanzibar.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb), akiongoza mkutano kati yake na viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Zanzibar, alipotembelea Mamlaka hiyo, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, visiwani Zanzibar.
Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Zanzibar, Bi. Khadija Issa Said, akielezea ufanyaji kazi wa Mfumo wa Bima wa TIRA MIS ambao ni wa kielektroniki unaorahisisha utoaji huduma na kudhibiti bima za kughushi, wakati wa mkutano kati ya viongozi wa Mamlaka hiyo Zanzibar na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (hayupo pichani).
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (wa tatu kulia) na Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Zanzibar, Bi. Khadija Issa Said (wa nne kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo Zanzibar, wakati wa ziara ya Naibu Waziri huyo ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima Zanzibar, Bw. Arafat Ally Haji, akieleza jambo wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb), alipotembelea Shirika hilo, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, visiwani Zanzibar.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (katikati), Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Zanzibar, Bi. Khadija Issa Said (wa tatu kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima Zanzibar, Bw. Arafat Ally Haji, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Shirika hilo, visiwani Zanzibar.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kushoto), akisikiliza maelezo ya Meneja wa Tawi la Bima la Mayfair, Bw. Livinus Mberwa, kuhusu utendaji kazi wa Kampuni, alipotembelea tawi hilo, visiwani Zanzibar.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (katikati), Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Zanzibar, Bi. Khadija Issa Said (wa pili kulia) na Meneja wa Tawi la Bima la Mayfair Zanzibar, Bw. Livinus Mberwa, wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa tawi hilo visiwani Zanzibar.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kulia), akisikiliza maelezo ya Meneja Mauzo wa Kampuni ya Strategis Insurance Zanzibar, Bw. Sabri Omar Ali, alipotembelea katika Kampuni hiyo, visiwani Zanzibar, katikati ni Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Zanzibar, Bw. Mohamed Khamis Ameir.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (wa tatu kushoto), Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Zanzibar, Bi. Khadija Issa Said (wa tatu kulia) na Meneja Mauzo wa Kampuni ya Strategis Insurance Zanzibar, Bw. Sabri Omar Ali (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kampuni hiyo ya Bima, wakati Naibu Waziri huyo alipoitembelea, visiwani Zanzibar.
(Picha na Peter Haule, WFM, Zanzibar)
*********************************
Na Benny Mwaipaja, Zanzibar
NAIBU Waziri wa Fedha na MIpango, Mheshimiwa Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa shughuli za Bima Nchini (TIRA) kusimamia kikamilifi Sheria ya Bima inayowataka waingizaji wote wa bidhaa Zanzibar kutoka nje ya nchi kukatia Bima mizigo yao kwa kutumia Kampuni za Bima zilizosajiliwa hapa nchini.
Mheshimiwa Masauni alitoa maagizo hayo alipofanya ziara katika Ofisi za Mamlaka hiyo Tawi la Zanzibar na kuzungumza na uongozi wa Tawi hilo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea na kukagua utendajikazi wa Taasisi zilizochini ya Wizara ya Fedha na Mipango Tanzania Bara na Zanzibar.
“Ni lazima TIRA isimamie kikamilifu Sheria hiyo ya Bima Namba 10 ya mwaka 2009, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017, inayosisitiza juu ya umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini zinakatiwa bima na Kampuni za Bima zilizopo Tanzania” alifafanua Mhe. Masauni.
Alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inasisitiza kutekeleza Sera ya Uchumi wa Blue, sehemu kubwa ya bidhaa zinazoingia Zanzibar zinategemea usafiri wa Baharini ni vema fedha inayotumika kukata Bima ibaki nchini badala ya nje ya nchi ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi.
Aidha ameipongeza TIRA kwa kuanzisha Mfumo wa TIRA MIS ambao unatumika kudhibiti kughushiwa kwa bima nchini, na kuongeza kuwa kwa kipindi kirefu kulikuwa na tatizo la watu kutengeneza bima za kughushi, hivyo ni imani yake kuwa kupitia Mfumo huo tatizo hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi.
Pia ameiagiza Mamlaka ya TIRA Zanzibar kuhakikisha inafuatilia kwa kina mwenendo mzima wa utendaji kazi wa Mfumo wa TIRA MIS ili uwe mbele kuliko mbinu za kiharifu.
Vilevile amewataka wananchi kuhakikisha wanatii Sheria sambamba na Mamlaka ya TIRA kufuatilia kesi zote zinazohusisha watu walioshiriki katika uharifu wa kutengeneza bima za kughushi na kujua hatima za kesi hizo na hatua zinachukuliwa kwa mujibu wa Sheria ili kutotoa mwanya kwa wenye nia ovu kughushi bima hizo.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa shughuli za Bima Tanzania (TIRA), Bi. Khadija Issa Said, amemshukuru Mhandisi Masauni kwa kutembelea Mamlaka hiyo Tawi la Zanzibar na kutoa nasaha na pia kujua changamoto zinazoikabili Mamlaka, aidha ameahidi kuwa Mamalaka yake itayafanyia kazi maagizo yaliyotolewa.
Naibu Kamishna Bi. Khadija Issa Said aliwataka wananchi watumie Mfumo wa TIRA MIS kukata bima na kujua uhalali wa zima zao, pia wametakiwa kupeleka malalamiko yao katika Mamlaka hiyo kuhusiana na bima walizokata ambazo zimewaletea usumbufu
Alisema kuwa TIRA Zanzibar ipo kwa ajili yao hivyo wasihadaike kwa kutumia Stika za Bima za karatasi zilizokuwa zinawekwa kwenye kioo cha chombo cha moto na badala yake watumie stika za kielektroniki ambayo inatokana na Mfumo wa TIRA MIS ambao unaweza kutambua uhalali wa bima kupitia Simu ya Mkononi.