Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akiwa pamoja na wajumbe walioshiriki Katibu Mkuu kikao cha kuanza utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Mkoani Simiyu, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akiongoza kikao cha kuanza utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Mkoani Simiyu, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza katika kikao cha kuanza utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Mkoa wa Simiyu (Simiyu Climate Resilience Project), jijini Dodoma.
Wajumbe wakizungumza katika kao cha kuanza utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Mkoani Simiyu, jijini Dodoma.
Mratibu wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Mkoa wa Simiyu (Simiyu Climate Resilience Project), Mhandisi Mwajuma Lugendo akitoa taarifa ya jinsi ya utekelezaji wa mradi kwa wajumbe walioshiriki kikao cha kuanza utekelezaji wa mradi huo, jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameongoza Kikao cha kuanza utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Mkoa wa Simiyu (Simiyu Climate Resilience Project) kilichohusisha uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), Wataalam Washauri kutoka Kampuni za GFA na GITEC-IGIP za Ujerumani, Wataalam wa Wizara ya Maji na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujadili utekelezaji wa mradi huo.
Majadiliano ya kikao hicho yalihusisha mpango mzima wa utekelezaji wa mradi huo utakaotekelezwa kwa gharama ya kiasi cha Euro milioni 171 zitakazotokana na michango ya Serikali ya Tanzania, Shirika la Green Climate Fund (GCF) na KfW kulingana na mkataba wa kifedha uliosaniwa Mei 3, 2019.
Katibu Mkuu Mhandisi Sanga amewataka wahusika wote katika utekelezaji wa mradi huo kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kusisitiza kuwa Serikali haitakubali kuidhinisha malipo ya ziada kinyume na mkataba. Amewataka wakandarasi watakaopata zabuni kukamilisha kazi kwa wakati na ubora.
“Ni muhimu kuwa na mawasiliano mazuri wakati wote wa utekelezaji na kuchukua maamuzi kwa wakati kwa pande zote, pamoja na kushirikiana kwa karibu na wakazi wa Simiyu katika kila hatua ili kuharakisha na kufanikisha utekelezaji wa mradi huu muhimu’’, amesema Mhandisi Sanga.
“Niwatake wataalam washauri, wakandarasi na wataalam wa wizara kuwa waaminifu kwa lengo la kufanikisha mradi huu kwa ajili ya wakazi wa Simiyu ambao kwa sehemu kubwa mazingira yao ni kame na kuleta chachu ya maendeleo kupitia huduma ya uhakika ya majisafi na salama”.
Mradi wa Maji wa Simiyu unatarajiwa kupeleka huduma ya majisafi, salama na ya kutosheleza katika wilaya zote tano za Busega, Bariadi, Itilima, Meatu na Maswa ikiwa na jumla ya wananchi 878,000 katika vijiji 250 mkoani Simiyu.
Mkataba wa kuanza kazi rasmi unatarajiwa kusainiwa mwezi Septemba, 2021 na utekelezaji wake utakuwa wa awamu mbili. Awamu ya kwanza itaanza na wilaya za Busega, Itilima na Bariadi, awamu ya pili itamalizia wilaya za Maswa na Meatu.
Aidha, mmoja wa Wakurugenzi Mtendaji wa GFA, Anja Desai amesema watasimamia vyema utekelezaji wa mradi kama Wataalam Washauri na kuhakikisha Serikali ya Tanzania inakabidhiwa kazi yenye ubora kulingana na mkataba.
Pamoja na kuishukuru ushirikiano ilioupata mpaka hatua iliyofakiwa, jambo linalotia moyo katika utekelezaji wa mradi huo.