Mbunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile ambaye amewaomba Wananchi wa Jimbo la Konde Pemba kumpigia kura za ndio Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi CCM kwenye Jimbo hilo, Shekha Fakhi Mpemba.
Ditopile ambaye ni miongoni mwa viongozi wa CCM waliofika Visiwani humo kuongeza nguvu katika kura za Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, amesema Shekha Fakhi Mpemba ndie Mtu sahihi ambaye anaweza kutatua changamoto za Wananchi wa Konde kwa haraka bila ubaguzi wa aina yeyote.
Amesema uwepo wa Mbunge wa CCM katika Jimbo la Konde kutaharakisha Maendeleo ya vitu na watu kwa haraka kwa kuwa ni rahisi kwake kuiishi ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo ndio inatekelezwa hivi Sasa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
” Ni lazima tuwe na kiongozi ambaye anazungumza lugha moja na Rais Dk Mwinyi, Mbunge ambaye mkononi mwake atakua ameshika ilani ya uchaguzi ya CCM kwa miaka mitano inayoeleza nini tutafanya katika sekta ya afya, maji, elimu na miundombinu, tusichague viongozi ambao wanataka kuingia kwa lengo la kutukwamisha.
Wananchi wa Zanzibar ni waelewa na Zanzibar ya leo siyo ya jana, tunajua viongozi wa kweli na wababaishaji, CCM kupitia kwa Mwenyekiti wetu Taifa, Makamu wake Zanzibar, wameona Shekha Fakhi Mpemba ndio Mtu sahihi wa kuwatumikia Wananchi wa Konde twendeni tukamchague kwa kura zote,” Amesema Ditopile.
Amesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kipindi kifupi ni kubwa na iliyotukuka ambayo kwa vyovyote vile inapaswa kuungwa mkono kwa kuhakikisha wanapata wabunge makini wenye uwezo wa kuishauri Serikali.
Jimbo la Konde linafanya uchaguzi wake mdogo Julai 18 mwaka huu ambapo CCM imemsimamisha Shekha Fakhi Mpemba kuwania kiti hicho baada ya aliyekua Mbunge wake Khatib Haji kufariki Dunia.