Home Mchanganyiko MAFUNZO YA UALIMU WA UFUNDI KUPITIA ELIMU MASAFA KUBORESHWA

MAFUNZO YA UALIMU WA UFUNDI KUPITIA ELIMU MASAFA KUBORESHWA

0

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo akipokea maelezo kutoka kwa Mkufunzi wa Fani ya Umeme katika chuo cha MVTTC, Frank Urio alipotembelea Maabara ya kufundishia fani umeme kwa walimu tarajali katika chuo hicho.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo akiongea na Uongozi na Wakufunzi wa chuo cha MVTTC (hawapo pichani), wakati alipotembelea chuo hicho hivi karibuni.

Baadhi ya Wakufunzi wa chuo cha MVTTC wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Prof. Carolyne Nombo (hayupo pichani) wakati alipotembelea chuo hicho hivi karibuni.

…………………………………………………………………

Na WyEST

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amekitaka Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kuongeza fursa za utoaji mafunzo ya ualimu wa ufundi stadi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji.

Ameyasema hayo Mkoani Morogoro alipotembelea Chuo hicho ambacho ni chuo pekee kinachotoa mafunzo ya ualimu wa ufundi stadi nchini, ambapo amekitaka kutoa mafunzo kwa kutumia mfumo wa elimu masafa na mtandao.

“Tusibaki tu kufundisha somo la Tehama bali tulitumie katika kufikia walimu wengi bila ya kuwa na ulazima wa wao kuja chuoni kupata mafunzo ya nadharia,” amesema Prof. Nombo.

Prof. Nombo pia ameutaka uongozi wa chuo hicho kuhamasisha watoto wa kike kusomea mafunzo ya ualimu wa ufundi stadi ili kuleta hamasa kwa watoto wa kike wengi zaidi kujiunga na mafunzo ya ufundi.

“Sasa hivi tunaongelea wasichana na akina mama katika sayansi na teknolojia, hivyo tunatakiwa kuwahamasisha kusomea ufundi stadi kwa kuwa na walimu wa kike wanaofundisha masomo hayo katika vyuo vyetu,” amesisitiza Prof. Nombo.

Naye Afisa Elimu Maalum Mkoa wa Morogoro Rhoda Sheba amemwomba Katibu Mkuu huyo kusaidia wanafunzi waliomaliza darasa la saba ambao wanasoma mafunzo ya ufundi stadi katika vituo vilivyopo katika shule za msingi mafunzo yao kutambulika ili waweze kuendelea na masomo katika vyuo vya VETA.

Awali Mkuu wa Chuo, Samwel Kaali amesema chuo chicho kinatekeleza mpango wa maendeleo wa miaka 10 ikiwemo kuendeleza watumishi wa kada zote, kuongeza udahili wa mafunzo kupitia mfumo wa elimu masafa na kuendeleza mafunzo ya stashahada ya ualimu.