…………………………………………………………………………………….
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.5 katika jimbo lake kwaajili ya ujenzi wa barabara za vijiji ambazo zinasaidia wananchi katika kusafirishia mazao ya biashara.
Hayo ameyasema alipokuwa kwenye mkutano katika kijiji cha Mlangali ndani kata ya Mlangali ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea wananchi wa vijiji mbalimbali vya jimbo lake kwa lengo la kusikiliza changamoto zao.
Mbunge huyo aliyesema hayo baada ya wananchi kulalamikia ubovu wa miundombinu mbalimbali ya barabara zinazounganisha vijiji na kata kuwa mibovu kiasi cha kushindwa kusafirisha mazao yao hasa barabara inayounganisha kata ya Milo na Mlangali hivyo wameomba msaada wa matengenezo.
Wananchi hao walidai kuwa wamekuwa wakishindwa kusafirisha mazao yao ya biashara kupeleka mijini kutokana na magari kushindwa kufika mahali yalipo mazao kitu ambacho kinawakatisha tamaa ya kufanya shughuli za kilimo.
Akizungumza mmoja wa wananchi hao Onesmo Msanga amesema kuwa katika kijiji cha Mlangali ndani wanalima mazao ya aina nyingi kama njegele, ngano, viazi, mbao na kadhalika hivyo ili waweze kuuza mazao hayo wanahitaji barabara zitakazowasaidia kusafirisha kwa urahisi.
Aidha kwa upande wa mbunge huyo amesema barabara nyingi za kuunganisha vijiji na kata tayari zipo kwenye mpango wa kuboreshwa na tayari baadhi ya barabara zimeanza kufanyiwa kazi.
Amesema barabara ambazo zimeanza kufanyiwa kazi ni yakutoka Madilu hadi Ilininda ambayo imewekewa bajeti ya kiasi cha shilingi milioni 250, barabara ya kwenda Milo ambayo inatengenezwa kwa urefu wa km 15 na inagharimu kiasi cha shilingi millioni 250.
Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa barabara hizo serikali imeamua kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuweza kuongeza bajeti kwa wakala wa barabara za vijijini (TARURA) ili waweze kuboresha barabara hizi.
” Wakulima wanazitegemea sana barabara hizi za vijiji katika shughuli zao za kiuchumi, siku chache zilizopita nilipigiwa simu na wakulima wa vitunguu kutoka kijiji cha Mbwila wakidai wamepata wateja wa vitunguu kutoka nchi jirani lakini wanashindwa kufika kutokana na miundombinu mibovu ya barabara”, Alisema Kamonga.
Amesema wananchi wanapaswa kuto nung’unika juu ya tozo za simu zinazotolewa na serikali ni kwaajili ya barabara hizo za vijiji zinazojengwa hivyo wananchi wanapaswa kuipongeza serikali kwani matumizi ya fedha zao yanaonekana.
Mbunge huyo mpaka sasa tayari ametembelea vijiji 19 ambavyo ni Kingole, Kiyogo, Lihagule, Lihighai, Lifua, Luilo, Kipangala, Idusi, Nkomang’ombe, Iwela, Muhumbi, Kimelembe, Ligumbilo, Lufumbu, Mlangali, Itundu, Utilili, Lusala na Lupanga.
Katika vijiji hivyo changamoto ambazo zimeonekana kujitokeza kwa vijiji vingi ni maji, barabara pamoja na huduma ya afya.