Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitatua changamoto za ardhi kwa wananchi waliojitokeza kuwasilisha kero zao katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya Mafiga katika manispaa ya Morogoro
Sehemu ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro wakiwa wamepanga mstari kwa ajili ya kusikilizwa kero zao za ardhi na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya Mafiga mkoani Morogoro
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela akizungumza wakati wa uwasilishaji kero za ardhi kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwenye mkutano wa hadhata eneo la stendi ya Mafiga Morogoro
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitatua changamoto za ardhi kwa wananchi waliojitokeza kuwasilisha kero zao katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya Mafiga katika manispaa ya Morogoro
………………………………………………………………….
Na Munir Shemweta, Morogoro
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesikiliza jumla ya kero 120 za ardhi ndani ya siku mbili na kuzipatia ufumbuzi baadhi ya kero hizo ikiwa ni utekelezaji wa magizo ya rais Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri Mabula ambaye alianza kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi juzi katika wilaya ya Kilosa na jana alikutana na wananchi wenye kero hizo kwenye mkutano wa hadhara eneo la stendi ya Mafiga katika manispaa ya Morogoro.
Akiwa ameambatana na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela, Katibu Tawala Mariam Mtunguja, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa Frank Minzikuntwe pamoja na Wataalamu wa sekta ya Ardhi kutoka manispaa ya morogoro, Naibu Waziri Dkt Mabula alimpa fursa kila mwananchi mwenye changamoto ya ardhi kuwasilisha kero yake kwa uwazi na kuwataka wahusika kujibu hoja za wananchi kabla ya yeye kutoa maamuzi.
Kero nyingi za ardhi zilizowasilishwa kwa Naibu Waziri wa Ardhi, zilikuwa ni malalamiko ya kudhulimiwa maeneo, umilikishaji ardhi mara mbili pamoja na udaiji fidia uliotokana na wananchi kuchukuliwa maeneo yao kutokana na shughuli za kimaendeleo ama umilikishwaji mara mbili.
Akizungumnza wakati wa kuzipatia ufumbuzi kero hizo ambazo baadhi yake ni za miaka ya tisini, Naibu Waziri Dkt. Mabula aliwataka wananchi kuwa makini wakati wa kununua ardhi na kuhakikisha kabla ya kufanya uamuzi wa kununua ardhi wanapata taarifa ofisi za ardhi kujua kama eneo husika limemilikishwa.
‘’Mnapotaka kununua eneo lazima mkaulizie katika ofisi za ardhi ili kujua kama eneo hilo limemilikishwa kwa mtu mwingine au matumizi ya eneo hilo ni yapi maana unaweza kuuziwa eneo kumbe ni la wazi’ alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi alitoa maelekezo kwa waendaji wa sekta ya ardhi kudhibiti ujenzi holela katika maeneo yao na kuhakikisha hakuna mtu anayejenga bila kuwa na kibali na ujenzi uzingatie mipango miji ya eneo husika.
‘’Lazima mdhibiti ujenzi holela katika halmashauri zenu na mshirikishe watendaji wa mitaa kwa kuwa zoezi la urasimishaji linaloendelea sasa siyo la kudumu na hatuwezi kufanya urasimishaji huku ujenzi holela unaendelea’ alisema dkt Mabula.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando alimpongeza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuweza kusikiliza kero 120 za ardhi ndani ya siku mbili na kusema hatua hiyo inaifanya wilaya yake kuongeza juhudi za kushughulikia migogoro ya ardhi tofauti na malengo yake ya kusikiliza kero mia tano kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Msando, wilaya ya Morogoro imejiwekea malengo ya kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi mia tano katika kipindi cha mwaka mmoja.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Frank Minzukuntwe alieleza katika mkutano huo kuwa, migogoro mingi ya ardhi kwenye mkoa huo imesababishwa na ununuzi holela wa ardhi unaofanywa na wananchi hasa kupitia watendaji mitaa au wenyeviti wa vijiji.
“Migogoro mingi hapa morogoro imesababishwa na wananchi kununua ardhi kiholela bila kupitia ofisi za ardhi ambazo ndizo zenye kumbukumbu za wamiliki” alisema Frank.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alimaliza ziara yake jana mkoani Morogoro na anaendelea katika mkoa wa Dodoma eneo la Kibaigwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyemtaka kwenda kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo.