Muonekano wa sehemu ya lambo kwa
ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu ambalo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amelikabidhi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Chalinze
baada ya kukarabatiwa na serikali kwa zaidi ya Shilingi Milioni 600 na kuagiza
kuundwa kwa kamati ya kusimamia lambo hilo. (Picha
na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Na. Edward Kondela
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameagiza shamba la
malisho ya mifugo lililopo Vikuge Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani,
kujiendesha kibiashara na kusambaza mbegu za malisho kutoka nchini China
ijulikanayo kama JUNCAO maeneo mbalimbali nchini kwa kuwa ina sifa ya
kustahimili sehemu yenye ukame ili wafugaji wapande malisho hayo.
Wakati
akihitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo Naibu Waziri
Ulega, amesema hayo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya shamba
hilo na kumuagiza Katibu Mkuu anayeshugulikia Mifugo Prof. Elisante Ole
Gabriel kuhakikisha aina mpya ya malisho hayo inasambazwa na kusimamia
vyema ili mradi huo uweze kuwa na tija kwa taifa hususan kwa wafugaji
vijijini.
Mhe. Ulega amesema mbegu za malisho ya JUNCAO
zisambazwe kuanzia ngazi ya mikoa wilaya hadi vijiji lengo likiwa
kudhibiti mifugo na wafugaji kuhamahama kutafuta malisho.
Amefafanua
kuwa hataki kuona mambo yanayoanzishwa kwa ajili ya kunufaisha wananchi
yanaishia njiani kwani ni vizuri kukawa na mwendelezo wa teknolojia
hiyo ya kilimo hicho kipya cha malisho ya mifugo hata kusambazwa kwa
wafugaji hadi vijijini.
Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha
mbegu za malisho hayo zinaenea hadi vijijini kwa wafugaji akitaja
hususan mikoa yenye ukame kama Dodoma, Singida, Manyara, Shinyanga na
iwapo zitasambazwa vizuri itapunguza tatizo la wafugaji na mifugo yao
kuhama hama kutafuta malisho ya mifugo yao.
“Kinachosababisha
wafugaji kuzunguka na kuhama hama ni kutafuta chakula cha malisho na
maji kwa ajili ya mifugo yao hivyo kama wafugaji watafikishiwa mahali
walipo itawasaidia wafugaji kuwa na uhakika wa malisho.” amesema Mhe.
Ulega.
“Mbegu hizi nataka zifike kwa haraka na kwa gharama nafuu
ambayo kila mfugaji ataweza kununua aweze kuhudumia mifugo yake.”
amesema Mhe. Ulega
Akizungumzia changamoto wanazokutana nazo
katika uendeshaji wa shamba la Vikuge Meneja wa shamba hilo Bw. Reuben
Ngailo amesema kukosekana kwa vifaa na nguvu kazi katika mipango yao ya
kusafisha shamba na kupanua uzalishaji.
Amesema pia eneo hilo la
shamba lina visiki vingi ili kuving’oa inagharimu kiasi kikubwa cha
fedha jambo ambalo husababisha kuendesha uzalishaji wa malisho katika
eneo dogo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe.
Ridhiwani Kikwete akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega ameomba malisho yanayozalishwa shambani hapo
kuwanufaisha wakazi wa Mkoa wa Pwani.
Mhe. Kikwete amesema shamba
hilo lipo Mkoa wa Pwani na mkoa huo una migogoro mingi ya wakulima na
wafugaji kwa ajili ya kutafuta malisho na maji, hivyo ombi lake ni mbegu
hizo zisambazwe haraka kwa wafugaji wa mkoa huo.
Katika hatua
nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amekabidhi
lambo la kunyweshea mifugo maji la Chamakweza lililopo Wilaya ya
Chalinze Mkoani Pwani na kuiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Chalinze
kuunda kamati kwa ajili ya kusimamia lambo hilo lililokarabatiwa na
serikali kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Milioni 600 kwa ajili ya
matumizi ya mifugo na binadamu.
Mhe. Ulega amesema ni wakati
sasa wafugaji kutumia vyema lambo hilo kwa ajili ya kuboresha mifugo yao
ambayo imekuwa ikikosa maji ya kunywa na kuwataka kubadilika na kuanza
kufuga kibiashara kwa kuwa na mifugo ambayo wanakuwa wanavuna kila baada
ya muda kwa kuuza kwenye viwanda vya kuchakata nyama badala ya kuwa na
mazoea ya kuwa na mifugo mingi ambayo haina tija kwao.
Amefafanua
kuwa lengo la serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona mfugaji ananufaika kupitia
mifugo yake kwa kufanya biashara na hatimaye kuongeza pato la taifa na
mfugaji mwenyewe.
Naibu Waziri Ulega tayari amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Pwani.