Naibu Waziri wa Kilimo,Mhe.Hussein Bashe akizungumza kikao na waigizaji wa mbolea kujadili ni namna gani wanaweza kutatua changamoto zinazowakabiri waigizaji hao na kutengeneza fursa.
****************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Serikali imewakikishia wasambazaji wa mbolea nchini kuwa gharama za usafirishaji wa mbolea kuanzia bandarini mpaka kwa wakulima hazitaongezeka ili kusaidia kupunguza gharama za mbolea kwa mkulima kutokana na kupanda kwa bei kwenye soko la dunia.
Ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Kilimo,Mhe.Hussein Bashe alipokuwa amekaa kikao na waigizaji wa mbolea kujadili ni namna gani wanaweza kutatua changamoto zinazowakabiri waigizaji hao na kutengeneza fursa.
“Tutafanya kila jitihada ya kusaidia gharama zile ambazo zinaanzia kwenye bandari ya Dar es salaam kwenda kwa mkulima Kalambo, gharama zile tuweze kuzipunguza ili tuweza kuondoa presha inayotoka nje”. Amesema Mhe.Bashe.
Amesema kwa sasa serikali ipo katika mazungumzo na shirika la reli la TRC na Tazara ili mbolea iweze kusafirishwa kwa njia reli lengo kikiwa ni kupunguza gharama kwa mkulima.
Aidha amewahakikishia wakulima wa mahindi na mpunga uwepo wa soko la uhakika kwani serikali itanunua mahindi yao kwa kiwango kitakachokuwa rafiki na kuweza kuwanufaisha kwa kilimo hicho.
Pamoja na hayo Mhe.Bashe ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA) pamoja na taasisi ya utafiti wa kilimo nchini (TARI), kutoa elimu ya kutosha juu ya mbadala wa mbolea kama mkulima atakosa mbolea ya Urea.
Bei ya mbolea aina ya Urea katika soko la dunia imepanda kwa wastani wa dola 560 kutoka 359 kwa tani.