Mwenyekiti wa Baraza la wazee Mkoa wa Shinyanga Mzee Faustine Sengerema akiongea na baadhi ya Wazee hawapo pichani walioshiriki kikao cha Baraza hilo leo Mkoani Shinyanga.
Baadhi ya Wazee walioshiriki kikao cha Baraza la Wazee cha Mkoa wa Shinyanga wakisoma dua kabla ya kuanza kikao chao leo leo Mkoani Shinyanga.
Viongozi wa Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga wakishiriki sala kabla ya kuanza kikao chao leo Mkoani Shinyanga.
………………………………………………………………………..
Anthony Ishengoma- Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati ameagiza TASAF Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha inawaweka wazee wote wasio kuwa na uwezo wanaingizwa katika mpango wa kunusuru kaya masikini ili kupitia mpango huo waweze kupata katika Bima ya Afya ya Afya iliyoboreshwa.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesema bado kuna wazee ambao bado wanafanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kunyanyaswa na kubaguliwa ikiwemo mauaji na kuendelea kuishi maisha magumu jambo ambalo linachangiwa na imani potofu katika jamii hivyo kuwataka vijana kuwalinda wazee hao ili waweze kuishi kwa amani kwani katika uzee binadamu anahitaji kupendwa.
Dkt. Sengati amesema hayo leo wakati wa ufunguzi wa kikao cha robo mwaka cha Baraza la wazee wa Mkoa wa Shinyanga na kuikumbusha jamii kutambua kuwa kadili mwili wa binadamu unavyozeeka ndivyo viungo vinavyochoka hivyo kufanya wazee kupata magonjwa nyemelezi kama vile kisukari, presha na magonjwa mengine.
Dkt. Sengati aliongeza kuwa Mkoa wake una jumla ya wazee 66,717 ambao kati yao wanaume ni 29,717 na wanawake 36,500 na kati ya hao wazee wenye Bima ya Afya iliyoboreshwa 20,545 akiitaja idadi hiyo kuwa ndogo sana ukilinganisha na idadi wazee iliyopo katika mkoa wa Shinyanga na kutaka watendaji kuendelea kuimiza wazee kujiunga na Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu.
Naye Mzee Anderson Lymo Katibu wa Wazee Mkoa wa Shinyanga amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuangalia zaidi suala matibabu ya wazee kwa kuwa suala la ukosefu wa dawa kwa ajili ya matibabu ya wazee katika vituo vya Afya bado ni changamoto kubwa kwa wazee hapa Nchini.
Mzee Lymo aliongeza kuwa pamoja na upatikanaji wa Bima za Afya kwa wazee haitoshi kwani changamoto iliyopo imekuwa ni upatikanaji wa madawa katika zahanati, vituo vya Afya na hata hospitali kubwa na changamoto kubwa zaidi inayowakumba wazee ni umasikini kwakuwa wengi hawana shughuli inayowapatia kipato.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Braza la wazee Mkoa wa Shinyanga Mzee Faustine Sengerema ameomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati suala la wazee kushirikishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwemo serikali za vijiji na maeneo mengine ili kuwawezesha wazee kupaza sauti na kutoa ushauri kwa maendeleo ya Taifa.
Mzee Sengerema alisema kuwa suala la wazee kushirika katika maamuzi mbalimbali linatokana na miongozo mbalimbali iliyopo lakini utekelezaji wake umekuwa haufanyiki hivyo kuwanyima wazee haki ya kushirikishwa katika masuala mbalimbali ya mstakabali wa Nchi.
Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga linakaa kwa siku moja kufanya kikao chake cha robo mwaka ikiwemo maandalizi ya uchaguzi wa Baraza jipya la wazee ambalo lina wawakilishi kutoka Halmashauri zote sita zinazounda Mkoa wa Shinyanga na mabaraza mengine kama hayo tayari yameundwa katika mikoa mbalimbali hapa Nchini.