***************************
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Ikiwa ni msimu wa mavuno wa zao la mahindi katika maeneo mbalimbali hapa nchini, wakazi wa kata ya Mlangali wilayani Ludewa mkoani Njombe wamelalamikia ugumu wa soko wa zao hilo na kuiomba serikali kuwatafutia soko la uhakika ili waweze kuona thamani ya zao hilo.
Malamiko hayo wameyatoa mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga alipofanya ziara ya kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi katika kata hiyo na kukutana na kilio hicho cha wananchi.
Wananchi hao wamedai kuwa kwa sasa wanauza debe moja la mahindi kwa shilingi elfu tatu hadi nne kitu ambacho ukipiga mahesababu ya gharama walizotumia haziendani na bei hiyo na hakuna wanachopata.
Luciana Wila ni mmoja wa wakulima hao amesema kuwa wanawaomba wakala wa taifa wa uhifadhi wa chakula (NRF) kuja mapema kununua mahindi hayo pia ikiwezekana wanunue kwa wingi tofauti na miaka mingine.
Amesema kuwa NRF wamekuwa wakiwatumia vyama vya ushirika katika kununua mahindi hayo na hupewa kiwango kidogo cha ununuzi ambapo wanapewa tani 40 mpaka 48 na tani hizo huchukuliwa kwa mkopo kitu ambacho kwa sisi wakulima tunashindwa kutimiza mahitaji yetu kwa wakati kutokana na kutolipwa fedha kwa kipindi husika.
Kwa upande wa mwanchi mwingine aliyefahamika kwa jina la Evaristo Kayombo amesema kuwa mkulima mmoja anaweza kuwa na gunia mia mpaka mia saba halafu vyama vya ushirika vinataka wapeleke kuuza kila mtu angalau gunia tatu kitu ambacho kwa mtu mwenye magunia mengi ya mahindi anakuwa hajafanya chochote.
” Kwakweli kilimo hiki kinatukatisha tamaa sana! Maana tunapata tabu kilimo tukitegemea tukivuna tutanufaika ikiwemo na kuwalipia ada watoto wetu lakini hakuna chochote tunachopata zaidi ya kuumia tu na kuhangaika ada za watoto”, Alisema Kayombo.
Aidha kwa upande wa Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema suala hilo amekuwa akilisemea mara nyingi bungeni sambamba na kukutana na waziri wa kilimo kumuelezea masikitiko hayo ya wananchi.
Ameongeza kuwa asilimia kubwa ya wananchi wake hutegemea kilimo cha mahindi katika kuendesha shughuli zao na kwa mkoa wa Njombe jimbo lake ndilo linaongoza kwa uzalishaji wa mahindi hivyo wanapokosa soko la uhakika hupelekea kushuka kwa uchumi wa eneo hilo.
Amesema anaendelea kupambana kutafuta masoko ili wananchi wake waweze kuuza na kuona faida ya kilimo hicho kwani wamekuwa wakipata tabu sana kuhudumia mashamba hayo.
“Mahindi ndiyo yaliyo nisomesha mimi mpaka nakuwa mbunge hivyo ni vyema wakulima hawa wakanufaika na mazao yao kwa kuuza kwa thamani inayozidi gharama walizotumia kwa kilimo”.
Amesema wamekubaliana kuunganisha nguvu na mbunge wa jimbo la Madaba Joseph Mhagama ambaye ni jimbo jirani yake ili watafute masoko ya mahindi ili wananchi waweze kuuza mazao yao.