Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji akizungumzia ushiriki wa Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam
Baadhi ya teknolojia za mashine mbalimbali za kisasa za Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) zikiwa katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam ambayo yamefungwa Julai 13 mwaka huu na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
Muonekano wa Banda la Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) zkatika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ambapo yamefanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam na yamefungwa Julai 13 mwaka huu na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
……………………………………………………………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) limewataka wajasiriamali ambao hawatambuliki wafike Ofisi za SIDO kwa ajili kupewa mafunzo ambayo yatawasaidia kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitathibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) jambo ambalo litawasaidia kupiga hatua kiuchumi.
Akizungumzia ushiriki wa Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji, amesema kuwa mwaka huu wamekuwa na washiriki wengi katika banda la SIDO tofauti na mwaka 2020.
Prof. Mpanduji amesema mwaka huu wameshiriki wajasiriamali 115 tofauti na mwaka na 2020 ambapo walikuwa na washiriki 88.
“Washiriki wamezingatia mafunzo yetu kwani wametengeneza bidhaa zenye ubora na kuweka katika vifungashio rafiki na kuzifanya bidhaa zao kuwa na mvuto” amesema Prof. Mpanduji.
Ameeleza kuwa washiriki wa mwaka huu wameweza kuleta bidhaa zenye ubora hali ambayo inaonesha wamepata mafunzo mazuri kutoka SIDO.
Pro. Mpanduji amesema kuwa kwa sasa SIDO wana teknolojia za kisasa ambazo zinauwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye ubora ikiwemo mashine za kutengeneza mifuko mbadala pamoja na kumenya viazi na kukata chips.
Prof. Mpanduji amesema kuwa SIDO wana mashine za kisasa za kutotoresha vifaranga ambayo inauwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kutokana inaweza kuhifadhi joto muda mrefu hata kama umeme ukiwa umekatika.
Hata hivyo amefafanua mwaka huu viongozi wengi wa serikali wamefanikiwa kutembelea banda la SIDO akiwemo Makamu wa Rais, makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali ikiwemo Viwanda na Biashara, Wizara ya Uvuvi pamoja viongozi kutoka serikali ya Zanzibar.
Prof. Mpanduji amebainisha kuwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango baada ya kutembelea banda SIDO amewapongeza kwa mafanikio makubwa katika maonesho ya Biashara ya Kimataifa sabasaba.
SIDO inavipatia huduma viwanda vidogo na vya kati ikiwemo Maendeleo ya teknolojia ya Viwanda, Mafunzo ya Uendelezaji wa Biashara pamoja na masoko na ushauri wa kifedha.
Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya sabasaba yamefanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam yamefungwa Julai 13 , 2021 na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ambapo yalifunguliwa Julia 5 mwaka huu na Makamu wa Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.