***************************
Na Mwandishi Wetu,
Songea
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira Hamad Chande, ametoa siku tatu kuanzia jana(leo) kwa uongozi wa Manispaa ya Songea,kulipa madeni ya vibarua wanaofanya kazi katika machinjio ya kisasa ya Shule ya Tanga.
Naibu Waziri Chande, ametoa agizo hilo jana wakati alipotembelea machinjio hayo akiwa katika ziara yake ya siku tatu katika mkoa wa Ruvuma kujionea utekelezaji wa utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji katika mkoa wa Ruvuma.
Akiwa katika machinjio hayo Naibu Waziri alipata malalamiko kutoka kwa baadhi ya vibarua wakilalamika kutolipwa stahiki zao tangu machinjio hayo yaliyopoanza kufanya kazi Mwezi Mei Mwaka huu.
Amesema, Serikali ya awamu ya sita haitaki kuona wala kusikia wananchi wake wanapata shida kutokana na uzembe wa baadhi ya watumishi wake ambao wanashindwa kwa makusudi kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.
“kwa kuwa mkurugenzi hapa hayupo basi nakuagiza mwakilishi wake hadi kufika tarehe 15 keshokutwa akikisheni mnalipa madeni yote mnayodaiwa,pia mkuu wa wilaya nakuomba fuatilia malipo ya hawa vijana,siyo ustaarabu hata kidogo mtu unampa kazi lakini wakati wa malipo unamzungusha hili siperndi lijitokeze tena”amesema.
Aidha,ameagiza kufanyiwa marekebisho kadhaa katika machinjio hayo ikiwemo mfumo wa maji taka na kuwapa vifaa vya usalama vijana wanaofanya kazi katika machinjio baada ya kushuhudia wakifanya kazi mbalimbali kama kuondoa damu sakafuni na kusafisha sehemu ya kinyesi cha wanyama wanaochinjwa bila ya kuvaa vifaa kinga.
Hata hivyo,ameipongeza Manispaa hiyo kwa uamuzi wa kujenga machinjio hayo na kusisitiza yatumike kwa ajili ya wananchi kupata nyama safi.
Mwenyekiti wa umoja wachinja nyama katika machinjio hayo Ased Ali amesema, changamoto katika machinjio hayo ni uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi kama vile visu,kofia ngumu,buti na wafanyakazi wachache, hivyo ameiomba Manispaa kuwapatia vifaa na kuongeza idadi ya watumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Mmoja wa vibarua katika machinjio hayo Josephat Mwambiga, amelalamikia kutolipwa stahiki zake tangu machinjio yalipofunguliwa
jambo linalowafanya waishi maisha magumu ikiwemo kutakiwa kuhama kwenye nyumba walizopanga kutokana na kushindwa kulipa kodi.
Kwa upande wake Kaimu Mhandisi wa ujenzi wa Manispaa hiyo Caroline Bernald amesema, mradi wa machinjio ulianza kutekelezwa kwa awamu mbili,awamu ya kwanza ulianza mwezi Julai 2017 na kukamilika Machi 2019 na awamu ya pili ulianza Januari 2020 na kukamilika Mwezi Desemba 2020 kwa gharama ya sh.5,748,799,559.00.
Amesema, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa machinjio imefanywa na Mkandarasi Girraf Investment Ltd kwa gharama ya sh.2,725,624,900.00 na kusimamiwa na Mhandisi Mshauri S&F Consultancy kwa gharama ya sh.232,260,000.00 na hivyo kufanya gharama ya mradi kwa kipindi hicho kuwa sh.2,957,884,900.00.
Amesema, awamu ya pili ya ujenzi umetekelezwa na Wakandarasi wawili ambao ni STUMAIK Engeneering Co Ltd ambaye alianza kazi mwezi Januari 2020 na kukamilisha Mwezi Desemba kwa gharama ya sh.950,593,823.00 na mpaka mradi kukamilika imetumika sh.717,312,580.00.
Kwa mujibu wa Mhandisi Caroline, katika kipindi hicho msimamizi wa mradi ni Mhandisi mshauri Bureau For Industry Cooperatin(BICO) kwa gharama ya sh.225,856,250.00 na ameshalipwa sh.218,370,000.00.
Ametaja kazi zilizofanyika ni kuingiza umeme na kufunga Transfoma,kuchimba kisima kirefu cha maji mita 100,kuchimba mabwawa ya maji machafu,shimo la kutupa nyama isiofaa kwa matumizi ya binadamu.
MWISHO.