Kamati ya Uongozi ya mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) inayoundwa na Makatibu Wakuu wa Wizara 15, wakiwa katika picha ya pamoja baada kufanya ziara ya kukagua mradi huo, Julai 13, 2021.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (katikati) akiwa na Kamati ya Uongozi ya Mradi wa Julius Nyerere(JNHPP), wakipata maelezo ya mradi kutoka kwa Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Mhandisi John Mgeni,(pili kulia) walipofanya ziara ya kukagua mradi huo, Julai 13,2021.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (wa pili kushoto)akisikiliza jambo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka,( wa pili kulia), wengine ni Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara ya Nishati, Edward Ishengoma( kushoto) na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uwekezaji wa TANESCO, Mhandisi Khalid James( kulia)wakati wa ziara ya Kamati ya uongozi ya mradi wa Julius Nyerere(JNHPP), Julai 13,2021.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akizungumza na Kamati ya uongozi ya mradi wa Julius Nyerere(JNHPP),(hawapo pichani) walipofanya ziara ya kukagua mradi huo, Julai 13,2021.
Viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati, wakifatilia maelezo ya utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere( JNHPP), kutoka kulia ni Mhandisi Salum Inegeja, Mkurugenzi wa Manunuzi Sharif Fadhili, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Ziana Mlau na Mhasibu Mkuu Michael Marando, wakati wa ziara ya Kamati ya uongozi ya mradi wa Julius Nyerere(JNHPP), Julai 13,2021.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka,(kushoto) akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Julius Nyerere(JNHPP),kwa Kamati ya uongozi ya mradi huo walipofanya ziara, Julai 13,2021.
Kamati ya Uongozi ya Mradi wa Julius Nyerere(JNHPP), wakitazama eneo la linalojengwa nyumba ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme walipofanya ziara ya kukagua mradi huo, Julai 13,2021.
Sehemu ya ujenzi wa daraja la kudumu ukiendelea, daraja hilo litakuwa la pili kwa ukubwa katika Mto Rufiji likitangulia na lile la Mkapa.
Ujenzi ukiendelea katika Mahandaki Tisa ya kupekeleka maji katika mitambo ya kuzalisha umeme katika mradi wa Julius Nyerere (JNHPP).
********************************
Zuena Msuya, Pwani
Kamati ya Uongozi ya Mradi wa Julius Nyerere inayoundwa na Makatibu Wakuu wa Wizara 15, imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali ameongoza kamati hiyo, Julai 13, 2021, wakati wa ziara ya makatibu wakuu hao ya kutembelea na kukagua mradi huo wa kufua umeme wa Megawati 2,115, kwa kutumia maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji, mkoani Pwani.
Akizungumza kwa niaba ya Makatibu wakuu hao, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu ya Rais Mazingira, Marry Maganga alisema kuwa wamefarijika sana kuona kasi ya utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 54 ya ujenzi wa maeneo muhimu ya mradi.
Maganga alisema kuwa Makatibu wakuu wote wanaohusika moja kwa moja na mradi huo, wanaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kuhakikisha kila kitu kinatekelezeka kwa wakati bila kikwazo chochote ili kuhakika kuwa mradi huo utakamilika kama ulivyopangwa Mwezi Juni 2022.
“Mradi huu unatekelezwa kwa fedha zetu wenyewe watanzania,sisi makatibu wakuu tunajukumu la kuusimamia ipasavyo katika utekelezaji wake kwa kuhakikisha kuwa kila kitu kinaenda kama inavyotakiwa kurahisisha utekelezaji wa mradi huo, kwa umoja wetu tunajivunia kuwa sehemu ya kutekeleza mradi huu”, alisema Maganga.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, aliwaeleza makatibu wakuu hao kuwa, kwa kuwa Wizara ya Nishati ndiyo msimamizi mkuu wa utekelezaji wa mradi huo itahakikisha inakuwa bega kwa bega na wizara jumuishi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Aidha Mahimbali alisema kuwa wataendelea kumsimamia ipasavyo mkandarasi aliyepewa dhamana ujenzi wa mradi huo ili atekeleze majukumu yake ipasavyo kama ilivyoelekezwa katika makubaliano ya mkataba wa utekelezaji.
“Utekelezaji wa JNHPP uko katika hatua nzuri ya ujenzi katika maeneo yote makuu, ikiwamo Kingo za Bwawa husika, Tuta kuu la Bwawa, Kituo cha Kuchochea Umeme pamoja na Nyumba ya kuendeshea Mitambo ya kuzalisha umeme, mwenzi Novemba mwaka huu tutaanza kujaza maji kwa ajili ya kuzalisha umeme kuanzia mwezi juni 2022, kamati ya uongozi pia imeridhishwa na kasi ya ujenzi”, alisema Mahimbali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka aliwataka watanzania kuvuta subira na kuwa na imani na serikali yao kwakuwa mradi huo unatekelezeka na utazalisha umeme kama ilivyokusudiwa.
Aliwaeleza watanzania kuwa mradi huo utakapokamilika utawezesha umeme kuwa mwingi, wauhakika na kwa gharama nafuu, vilevile hata kuuza nje ya nchi wa watakaohitaji.
Kamati hiyo ilitembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa Mradi huo ambayo ni Handaki la Kuchepusha Maji ya Mto, Kingo za Bwawa husika, Tuta kuu la Bwawa, Kituo cha Kuchochea Umeme pamoja na Nyumba ya kuendeshea Mitambo ya kuzalisha umeme.
Aidha walitembelea na kukagua Daraja la Kudumu, Barabara, Njia ya kupitisha maji ya kuzalisha umeme, pamoja na eneo la ufungaji wa mitambo.