Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mussa Sima, akifurahi na viongozi na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo aliyoianza juzi.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mussa Sima, akizungumza na wananchi katika ziara hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mussa Sima akiserebuka katika ziara hiyo.
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakimuunga mkono mbunge kwa kutoa saruji baada ya mbunge huyo kutoa matofali 3000 kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mussa Sima akionesha Tuzo aliyotunukiwa na CCM na Serikali kutokana na mchango wake wa maendeleo kwa jamii.
Ziara ikiendelea kwa kuzungumza na wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mussa Sima, akikabidhi vifaa vya michezo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MBUNGE wa Jimbo la Singida Mjini Mussa Sima amefanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuwashukuru wananchi wa Kata ya Unyianga kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali.
Katika ziara hiyo Sima alitembelea Barabara ya kindai-Unyianga-mtamaa pamoja na Barabara ya Unyianga-Mwankoko na kujioneo ubovu wa Barabara hizo.
Kutokana na hali hiyo Sima aliwaeleza na kuwatoa hofu wananchi kuwa Barabara hizo zitajengwa muda mfupi kwa kuwa fedha tayari zimekwishatengwa hivyo wasiwe na wasiwasi kutokana na changamoto hiyo kwani inaenda kuondoka.
Sima alipata fursa pia ya kutembelea ujenzi wa kituo cha afya ambacho Serikali kwa mwaka huu mpya wa fedha imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi huo na kupongeza kasi inayoendelea ya ujenzi ambapo akaunga mkono kwa kuchangia tofali 3000, huku akichangia tofali 1000 kwa ajili ya ujenzi wa Shule shikizi Unyianga.
Sima pia alitoa vifaa vya michezo kwa kata zote za jimbo hilo kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Sima (SIMA CUP) yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo ya Unyianga Geofrey Mdama alimshukuru Mbunge kwa jinsi anavyowajali wananchi wa kata hiyo na kuunga mkono utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya pamoja na Serikali wamemtunuku hati za pongezi na shukrani Mbunge huyo kwa jinsi anavyotekeleza shughuli za maendeleo.