Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo Ofisi ya Rais TAMISEMI Philbert Rwakilomba akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu maandalizi ya ‘TAMISEMI QUEENS’ ambayo yamepangwa kufanyika Arusha kuanzia jumapili ijayo.
Baadhi ya Wachezaji wa ‘TAMISEMI QUEENS’ wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kushiriki ligi daraja la kwanza Netiboli kwa Tanzania Bara na Ligi ya Muungano
***************************
Na Mathew Kwembe, Dodoma
Timu ya netiboli ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ‘TAMISEMI QUEENS’ imejigamba kufanya vizuri katika michuano ya netiboli ligi daraja la kwanza iliyopangwa kufanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 18 hadi 29 julai 2021.
Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo ya TAMISEMI Philbert Rwakilomba amesema kuwa timu yake imejiandaa vizuri kwenye michuano hiyo hasa baada ya mwaka jana kushindwa kushiriki kutokana na janga la Korona.
Amesema kutokana na ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa viongozi wa juu wa wizara, hasa Waziri wa Nchi Mhe.Ummy Mwalimu na Katibu Mkuu Profesa Riziki Shemdoe, timu hiyo imepata maandalizi ya kutosha ya kuiwezesha kushiriki ligi hiyo na hatimaye kulibeba kombe hilo.
Rwakilomba amesema katika mojawapo ya maandalizi ya ligi hiyo tayari timu hiyo imeshiriki na kuwa mabingwa wa ligi ya Netiboli mkoa wa Dodoma mwaka huu.
Mwaka 2019 wakati mashindano hayo yalipofanyika jijini Dodoma ‘TAMISEMI QUEENS’ ilishika nafasi ya nne, huku JKT Mbweni akiwa bingwa wa mchezo wa netiboli Tanzania Bara na nafasi ya pili na tatu zikichukuliwa na Jeshi Stars, na jiji Arusha.
Katika ligi ya Netiboli TAMISEMI QUEENS ilizifunga timu za Cocacola, Jiji la Dodoma, Jiji la Tanga, SMART, Eagle, JKT Makutupora na ilipoteza michezo mitatu dhidi ya Mbweni JKT, Jeshi Stars na Jiji la Arusha.
Kwa upande wake Katibu wa TAMISEMI Sports Club Alex Ntenga ameahidi kuwa timu yake itazichapa timu zote itakazokutana nazo katika michuano hiyo wakiwemo Mbeni JKT na Jiji Arusha.
Katika michuano hiyo TAMISEMI QUEENS itawategemea wachezaji wake machachari Lilian Jovin, Flora Odilo, Rose Makange na Nahodha wa timu Dafrosa Luhwago huku kocha wa timu ni Maimuna Kitete.
Naye Afisa Michezo wa Jiji la Arusha Benson Maneno amesema timu ya Jiji Arusha, maarufu kama ‘Arusha City Queens’ imepanga kufanya vizuri katika michuano hiyo, ambapo hivi sasa ipo nje ya nchi kwa maandalizi.