………………………………………………………………
Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewataka maafisa habari wa wizara zote nchini kuwa wabunifu katika kazi zao ili waendane na mabadiliko ya teknolojia.
Msigwa ametoa maelekezo hayo jana jijini Dodoma alipokutana na Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara zote kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali namna ya kuboresha vitengo hivyo katika utoaji wa taarifa za serikali.
“Kazi zetu zinahitaji sana ubunifu, tuwe wabunifu, unaweza kupata mafunzo lakini kama huna ubunifu utabaki vilevile.
“Kimbizaneni na teknolojia, teknolojia zinabadilika kila siku, usisubiri mtu aje akufundishe, jifundishe mwenyewe kwanza.
“Hizi simu tunazotumia zina mambo sana, zitumieni vizuri, mafunzo tutawapa lakini changamkeni wenyewe kwanza, ameelekeza Msigwa.
Pamoja na hilo, amewataka maafisa habari hao kutunza kumbukumbu za kazi zao ili vizazi vinavyokuja viweze kuona kazi walizokuwa wakizifanya.
“Hii maktaba ya mtandaoni sio mbadala wa maktaba ya kawaida, hizi za mtandaoni mtu anaweza kuzifuta mara moja, tuwe nazo lakini tusiache njia za kawaida za utunzaji kumbukumbu,” ameagiza Msigwa.
Mwaka 2005 Serikali ilianzisha Vitengo vya Mawasiliano Serikalini ili taarifa za shughuli za Serikali ziweze kuwafikia wananchi ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha taasisi za Serikali zinatenda shughuli zake kwa uwazi ili kuimarisha demokrasia nchini.