Diwani wa Kata ya Makilawa Shaban Mtakii akizungumza kwenye kongamano hilo.
Amir wa Kanda ya Kaskazini, Swalahudini Ayoub, akizungumza kwenye kongamano hilo.
Boniphace Jilili na Dotto Mwaibale,Singida.
KAIMU Sheikh wa Mkoa wa Singida Issa Nassoro amezitaka taasisi zote za dini ya kiislamu kuacha malumbano na mafarakano badala yake washirikiane katika kumwabudu Mungu kwani wao ni kitu kimoja.
Sheikh Nassoro alitoa wito huo juzi wakati akifunga kongamano la kimataifa la waislamu lililofanyika katika kijiji cha Mtavira Kata ya Makilawa Wilaya ya Ikungi mkoani hapa.
Kongamano hilo lililofanyika kwa siku tatu kuanzia Ijumaa hadi jumapili liliwakutanisha kwa pamoja waumini wa dini ya kiislamu kutoka Kenya, Zanzibar na mikoa yote ya Tanzania Bara.
Alisema nchi yoyote,familia yoyote ama misikiti yoyote ikiendeleza ugomvi ama malumbano hakutakuwa na maendeleo..waislamu wapendane ugomvi hauna faida yoyote.
“Waislamu acheni magomvi,mtagombana mpaka lini..?mpaka lini tutaendelea kufarakana..? tuitafute pepo ya Mwenyezi Mungu kwa kufanya yaliyomapenzi yake,natarajia kongamano hili linakwenda kubadilisha mienendo yetu.” alisema Sheikh Nassoro.
Aidha Sheikh Nassoro alitumia fursa hiyo kuwashukuru Viongozi wa Serikali mkoani hapa hususani Mkuu wa mkoa kwa kutoa kibali ili kongamano hilo liweze kufanyika katika eneo hilo tena bila ya bughudha ama changamoto yoyote.
Awali kabla ya kumkaribisha kaimu Sheikh wa mkoa kiongozi mkuu wa Taasisi ya Fiysabili lahi Tabligh Markaz (F.T.M) yenye makao yake makuu Gongolamboto da er salaam ambao ndio waratibu wa kongamano hilo Sheikh Abdallah Swalihina Abubakari alisema wanafanya makongamono hayo kwa lengo la kuwaweka waislamu pamoja.
Aliwaomba waislamu kushirikiana na kuungana na taasisi zote za kiislamu zinapokuwa na shughuli yoyote ya kimaendeleo kama vile ujenzi wa misikiti ama shule za kiislamu kuchangia ili kufanikisha shughuli husika kwani wanajenga nyumba mmoja.
Alisema baada ya kuhitimishwa kongamano hilo mkoani hapa tayari maandalizi ya kongamano lingine yanafanyika mkoani Geita ambapo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha waislamu wote kwenda kushiriki na wenzao wa Geita na kwamba makongamono hayo yataendelea kufanyika maeneo mbalimbali kadri itakavyokuwa inapangwa.