……………………………………………………….
Na Gift Thadey, Babati
MBUNGE wa viti maalum (Vyuo vikuu) Dk Pauline Nahato, ametimiza ahadi yake kwa kukabidhi mapipa 10 ya kuhifadhi takataka kwenye Mji wa Babati Mkoani Manyara, katika maadhimisho ya wiki ya kutunza mazingira ya ‘Safisha Kitaa’.
Dk Nahato amesema ametimiza ahadi aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa tamasha la ‘Safisha Kitaa’ aliyoitoa kuwa atakabidhi mapipa 10 ya kuhifadhi taka, yatakayowekwa kwenye baadhi ya mitaa ya mjini Babati.
Aliwapongeza wana Babati kwa kuitikia kampeni ya ‘Safisha Kitaa’ kwani kwa namna moja au nyingine imefanikisha usafi wa mazingira kwenye baadhi ya mitaa ya mji huo.
“Kufanya usafi iwe utamaduni wetu wa kila siku kwani kila mmoja akitimiza wajibu wake katika kufanya usafi mji wetu wa Babati utazidi kupendeza na mazingira kuwa mazuri,” amesema Dk Nahato.
Amesema afya ikiimarika uchumi pia unakua hivyo usafi ni msingi wa afya wa kila mmoja na mazingira yakiwa safi magonjwa yanakuwa mbali na jamii inayowazunguka.
Mkurugenzi wa Mji wa Babati, Fortunatus Fwema akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, amewapongeza waandaji wa tamasha hilo.
“Pamoja na kusafisha mazingira kupitia kauli mbiu ya ‘Safisha Kitaa’ tumeona vijana wakifanya mazoezi kupitia michezo mbalimbali iliyochezwa,” amesema Fwema.
Kada maarufu wa CCM wa mkoa wa Manyara, Cosmas Masauda, amesema Dk Nahato ni mzalendo wa mji wa Babati kutokea eneo la Bonga hivyo wanampongeza kwa hatua hiyo.
“Dk Nahato amedhihirisha msemo wa nyumbani ni nyumbani kwa kitendo chake cha kununua mapipa 10 ya kuhifadhi taka na kugawa maeneo mbalimbali ya mitaa ya Babati,” amesema Masauda.