*********************
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
DIWANI wa viti maalum, Kibaha Mjini , Lidya Mgaya ametoa rai kwa kundi la vijana wakiwemo wa vyuo vikuu wajikite kujiendeleza kitaaluma pamoja na kuandaa miradi ili kujitegemea badala ya kusubiria kuajiriwa .
Aidha amewataka wakimbilie fursa ya kupata mikopo kupitia halmashauri zao kwani inaonekana kundi hilo la vijana na wenye ulemavu yapo nyuma kujiunga vikundi na kwenda kuomba mikopo hiyo isiyo na riba .
Akizungumza katika baraza la vijana kata ya Tumbi ,lililojumuisha viongozi wa vyuo vikuu na kata nyingine ,Lidya aliwataka vijana wakimbilie fursa ya ujasiliamali kuwa na miradi midogo midogo itakayo wasaidia kujiajili .
“Jiungeni vikundi ili kuendeleza miradi ama biashara kwa umoja kwa lengo la kupata mikopo kirahisi ,na vijana wa vyuo vikuu fuateni vigezo ,andaeni katiba zenu ,wazo la mradi ,ili muondokane kuwa mzigo baada ya kutoka vyuoni “
“Wapo baadhi ya vijana wanajisomesha ,wanajiendesha kimaisha wakiwa vyuoni kwa kutegemea biashara zao wakiwa shule ,hivyo inawezekana kufanya biashara zenu mkiwa chuo ili mkimaliza chuo msiwe mzigo kwa wazazi mkisubiria ajira za serikali ama kuajiliwa katika taasisi binafsi” alieleza Lidya.
“Kundi la wenye ulemavu ,vijana hawajitokezi sana unakuta fedha hizi zinarudi ,kundi la wanawake wanajitahidi mno ” alifafanua Mgaya.
Kwa upande wa viongozi kutoka vyuo vikuu ,walitaka kujua kama wanaweza kukopeshwa maana wanachojua wanakopeshwa vijana waliojiajili uraiani .
Pia waliomba serikali iongeze umri kwa kundi la vijana kuweza kukopeshwa kutoka miaka 35 hadi 38 maana unakuta wapo wengine miaka 35 inawaishilia wakiwa wanajiendeleza kitaaluma.
Vijana wa kata ya Visiga , Pangani na Tangini walielezea,wamenufaika na mikopo na kuwahakikishia wenzao wasipoteze hiyo fursa ya mikopo isiyo na riba na walisisitiza vijana waendeelee kupewa vitendea kazi kama pikipiki bajaji na sio pesa