…………………………………………………………….
Na. Damian Kunambi, Njombe
Wakazi wa vijiji mbalimbali vya kata ya Luilo pamoja na Masasi wilayani Ludewa mkoani Njombe wamelilalamikia shirika la umeme (TANESCO) wilayani humo kwa kutowafungia transifoma ambazo ziliondolewa kutokana na kupigwa na radi kwa takribani miezi mitano sasa na kupelekea kusimama kwa shughuli mba;imbali zinazotegemea umeme.
Malalamiko hayo wameyatoa katika ziara ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga alipowasili katika vijiji vya kata ya Masasi na Luilo kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi ili aweze kuzitatua na kuzifikisha mahala husika.
Wakiongea kwa masikitiko wananchi hao wamesema kuwa wanashindwa kuelewa sababu zinazofanya transifoma hizo zisifungwe kwa kipindi hicho kirefu hivyo wanamuomba mbunge huyo awasidie ili waweze kupata umeme.
Boniface Mbawala ni mmoja wa wananchi hao ambaye ni mkazi wa kata ya Masasi kijiji cha Kingole amesema tatizo hilo linawaathili kwa sehemu kubwa sana kwani kuna zahanati, shule, nyumba za ibada na taasisi nyingine za serikali ambazo zinahitajika kuwa na umeme muda wote ili huduma ziwe bora lakini kutokana na tatizo hilo la umeme hupelekea kupata huduma hafifu kuliko inavyotakiwa.
Ameongeza kwa kusema kuwa hali hiyo inawasononesha sana na wanaona kama serikali imewatupa haina mpango wa kuwasidia hata katika huduma ambazo wamezilipia.
“Hivi serikali imetuweka katika kundi gani sisi? Maana huduma ya umeme tumeilipia vyema sasa kwanini hatupewi huduma tunayotakiwa kupatiwa, tunaomba tuletewe transifoma ili tuendeshe shughuli zetu kama awali”, Alisema Mbawala.
Mahalamisi Upendo ni kikundi cha ngoma kilichopo katika kijiji cha Kipangala kata ya Luilo ambacho kinamiliki mradi wa mashine ya kukamua mafuta ya alizeti ambapo mashine hiyo huudumia wananchi kwa zaidi ya asilimia 90 wa tarafa ya Masasi wamesema kukosekana kwa umeme ni pigo kubwa kwao.
Carlolina Haule ni mwenyekiti wa kikundi hicho amesema kuwa mradi huo ulikuwa unawaingizia kipato ikiwemo na kuwasaidia wananchi wa maeneo mbalimbali wa tarafa hivyo kwa sasa wakazi hao wanakosa huduma kutokana na tatizo hilo la umeme
Akielezea sababu za kuchelewa kufungwa transifoma hizo meneja wa Tanesco wilayani humo Reuben Sichone amesema transifoma zote tisa zilichukuliwa na mkandarasi kwaajili ya kufanyiwa matengenezo na mpaka sasa transifoma nne kati ya tisa zilizoharibika amefanikiwa kurejesha huku tano zilizobakia zikiendelea kufanyiwa matengenezo.
Aidha kwa upande wa mbunge huyo amewapongeza wanakikundi hao kwa uwekezaji huo ambao unawasaidia wananchi kwa sehemu kubwa hivyo ni lazima atahakikisha transifoma hizo zinafungwa kwa haraka ili waathiriwa wote wanaondokana na adha hiyo wanayopata.
Hata hivyo amesema kuwa changamoto hiyo tayari alishaanza kuitafutia ufumbuzi ambapo aliongea na waziri wa nishati na madini Medad Kalemani na kumueleza shida wanayopata wananchi wake ambapo waziri huyo alizipokea na kutoa maelekezo kwa uongozi wa Tanesco mkoa pamoja na wilaya na amewapa muda mfupi wa kukamilisha utekelezaji huo.
“Ni lazima tuwaonyeshe kwa vitendo wananchi wetu kuwa hamkufanya makosa kukichagua chama cha mapinduzi kwakuwa chama hiki kipo kwa aajili ya kutatua shida zenu na ndiomaana mimi mbunge wenu kwa kushirikiana na madiwani wote tunakuwa karibu nanyi ili msipate shida wakati viongozi wenu tupo”, Alisema Kamonga.