Picha na Muhidin Amri
……………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Madaba
HALMASHAURI ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma,imekutana na wadau mbalimbali kwa mara ya kwanza tangu ianziswe june 5, 2016 ili kupata maoni yatakayosaidia kuboresha mpango mkakati na kuharakisha maendeleo ya Halmashauri.
Mpango huo unalenga kuleta mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya watu kutoka uchumi wa kati kwenda uchumi wa juu katika kipindi cha miaka mitano 2021-2026.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda amesema hayo jana, alipokuwa akitoa taarifa ya maandalizi ya mpango huo kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanya biashara,wawakilishi wa wakulima,viongozi wa Madhehebu ya Dini na taasisi za fedha.
Amewaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa,mpango mkakati wa miaka mitano ni mwelekeo wa Halmashauri katika kusaidia taasisi kuamua nini na wapi wanataka kufika ikiwa ni pamoja na hatua muhimu za kuchukua katika kuandaa mpango huo.
Mpenda amesema,Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuleta mabadiliko kwa kuboresha maisha ya Watanzania,kwa hiyo wanatakiwa kubadilka kifikra kwa kufanya kazi kwa nguvu na uzalendo ili kuondoa vikwazo vinavyosababisha umaskini.
Amesema,katika kutekeleza mpango huo watazingatia Sera za Kitaifa ikiwemo Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020-2025 na ushiriki wa jamii yenyewe,uboreshaji wa huduma na kupunguza umaskini wa kipato.
Mpenda amebainisha kuwa,mpango huo umeanisha kwa nini Halmashauri ipo,malengo waliyonayo,matarajio ya wadau katika utoaji wa huduma na namna ya kupima utendaji kwa watumishi na viongozi wake.
Mpenda amesema,kupitia mpango huo Halmashauri inaweza kuchangia katika ukuaji wa uchumi na kumaliza upungufu wa miundombinu katika huduma za kijamii kama vituo vya kutolea huduma za afya,madarasa.
Aidha, ametaja nyumba za watumishi,ofisi za vijiji, viwanda vidogo, vya kati na vikubwa,kuongeza mapato ya ndani,mifumo ya masoko,mipango na matumizi bora ya ardhi,biashara na kurahisisha usafiri na mawasiliano.
Kwa upande wake afisa mipango wa Halmashauri ya Madaba Mwandishi Nchimbi amesema, katika kipindi cha miaka mitano Halmashauri imefanikiwa katika mambo mbalimbali ikiwemo kutambua ardhi yote katika vijiji,ujenzi wa nyumba sita za wakuu wa idara,nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji na jengo la utawala.
Ametaja miradi mingine iliyotekelezwa katika kipindi hicho ni ujenzi wa nyumba mbili za watumishi katika vituo vya afya, kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2016/2017- 2019/2020, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka shilingi milioni 584,245,000 hadi kufikia milioni 879,750,524 sawa na asilimia 92 ya lengo kwa mwaka wa fedha 2020.
Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema, ameipongeza Halmashauri ya Madaba kwa kuandaa mpango mkakati ambao unakwenda kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa Halmashauri na wananchi wa jimbo la Madaba.
Amesema, Halmashauri ambayo haina mpango mkakati ni kama inakwenda kwa kupapasa haina mwelekeo na kamwe haiwezi kupata mafanikio ya kiuchumi na maendeleo ya watu wake.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya,Halmashauri ya Madaba kupitia mkakati huo inakwenda kukua na kuwa kitovu cha kibiashara sio kwa mkoa wa Ruvuma tu bali nchi kwa jumla hasa kutokana na Serikali kuwa kwenye mpango wa ujenzi wa Reli ya kisasa kutoka Mtwara kwenda Bandari ya Mbambaby wilaya ya Nyasa ambayo itakuwa na vituo viwili,kimoja kitakuwa Madaba na kingine Songea.