…………………………………………………………………………
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi, amewataka baadhi ya Wabunge,Wawakilishi na Madiwani wanaogombana na kuendeleza migogoro katika majimbo yao kuacha tabia hiyo.
Angalizo hilo amelitoa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani na kuimarisha uhai wa Chama katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema Viongozi wana jukumu la kuwatumikia wananchi hivyo hawana sababu ya kutofautiana na kuanzisha migogoro isiyokuwa ya lazima katika maeneo yao.
Alifafanua kwamba kuna baadhi ya viongozi wa majimbo nchini wamekuwa na migogoro ya kugombana wenyewe kwa wenyewe badala ya kuwatumia wananchi hali inayokwamisha maendeleo ya majimbo hayo.
Kuptia ziara hiyo alitoa onyo kali kwa kueleza kwamba CCM haiwezi kuwavumilia viongozi wa aina hiyo na haitosita kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi yao kwani waliomba ridhaa ya uongozi huo kwa maamuzi yao bila kulazimishwa.
“Kupitia maelekezo ya vikao vikubwa vya Kamati Kuu ya CCM Taifa tumeelekezwa tuwakumbushe viongozi wote wa ngazi mbalimbali wakiwemo Wabunge, Wawakilishi na Madiwani kushuka kwa wananchi kusikiliza hoja,ushauri na changamoto zao kasha kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Kwa maelekezo hayo hatutakuwa na nafasi ya kuwavumilia baadhi ya viongozi wanaochelewesha maendeleo hasa kwa ngazi ya majimbo na maeneo mengine ya umma ni lazima tuchukue hatua kali dhidi yao, tunahitaji kuona majimbo yote yanaondoana na changamoto na kuwa majimbo yaliyopiga hatua kubwa za maendeleo.”, alisema Dk. Mabodi.
Dk. Mabodi, aliwapongea Wabunge na Wawakilishi wa majimbo ya Mkoa huo kwa juhudi zao za kuwatumikia wananchi na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM katika maeneo mbalimbali majimboni mwao.
“Kasi ya utendaji wenu inaridhisha kwani changamoto nyingi zinazowakabili wananchi mmekuwa mkizitatua kwa wakati, jambo linaloongeza imani kwa wananchi wenu ambao ndio waliowapa ridhaa ya kuongoza katika maeneo yenu endeleeni kuchapa kazi.”, alisema Dk. Mabodi.
Pamoja na hayo Dk. Mabodi, alisema lengo la ziara hiyo ni kukutana na mabalozi wa mashina ya CCM kubadilishana nao mawazo sambamba na kusikiliza hoja zao kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na mabalozi hao aliwambia kwamba CCM inathamini uwepo wao kwani ndani ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 imetaja kuwa wao ndio wanachama namba moja.
Alisema mabalozi hao wapo karibu na wananchi hivyo wanatakiwa kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kikatiba ambao ni kulinda na kuendeleza Siasa ya CCM katika shina pamoja kutekeleza ipasavyo maamuzi na maagizo ya ngazi za juu ya CCM na ya Serikali na shughuli zingine za umma.
Kupitia ziara hiyo Dk. Mabodi, aliwasisitiza mabalozi hao kuendelea kufanya vikao vya kikatiba ili kujua mwenendo wa jamii husika pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika maeneo yao.
Alisema ushindi wa Chama katika uchaguzi Mkuu wa Dola uliopita wa mwaka 2020, umetokana na juhudi kubwa za kiutendaji zilizofanywa na Mabalozi wa mashina katika maeneo mbalimbali nchini.
“ Chama Cha Mapinduzi kinawashukru sana kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuhakikisha tunashinda ushindi wa kihistoria katika uchaguzi mkuu uliopita, tunaelewa mnafanya kazi kwa kujitolea lakini mmekuwa mkijituma sana katika kulinda maslahi ya CCM.”,aliwapongeza Dk. Mabodi.
Alisema madhumuni ya CCM ni kuendelea haki na usawa kwa wananchi wa ngazi zote hasa wa vijijini ili nao wapate huduma bora kama zinazopatikana katika maeneo ya mijini.
Alieleza kwamba utamaduni wa kuonana na wanachama wa mashina na matawi kila ikikaribia uchaguzi umekwisha, badala yake kwa sasa Chama kimewaagiza viongozi wa ngazi zote wakiwemo Wabunge na Wawakilishi kushuka kwa wananchi kusikiliza hoja zao na kutafuta ufumbuzi wake.
Kwa upande wake Balozi wa shina namba tatu wa Tawi la CCM Bungi Charles Kagumila Mayunga, alisema amefurahi sana kutembelewa na viongozi wa ngazi za juu hatua inayoonyesha uimara wa Chama kwa viongozi kushuka kwa wananchi wa ngazi za chini.
“Sio kawaida kuona kiongozi mkubwa kama Naibu Katibu Mkuu wa Chama chetu kuja katika shina kuzungumza na wanachama hasa wajumbe wa mashina hii haya ni mabadiliko makubwa ya kiutendaji ambayo yanatupa moyo wa kuendelea kujituma zaidi.”, alisema Charles.
Wakiwasilisha Changamoto mbalimbali mabalozi wa mashina ya CCM wa Mkoa huo walisema bado wanakabiliwa na changamoto za ubovu wa barabara za ndani, upungufu wa madarasa kwa baadhi ya skuli, ukosefu wa huduma za maji safi na salama, baadhi ya maeneo kutofika kwa huduma za umeme pamoja na uwepo wa bei ndogo za zao la Mwani.
Katika ziara hiyo Dk.Mabodi, alikagua miradi ya ujenzi wa madarasa matano ya Skuli ya Msingi na Sekondari Tunguu pamoja na uchongaji wa barabara mpya ya ndani inayotoka katika kijiji cha Mjonga nda Tunguu Polisi yenye urefu wa kilomita 3.02.
Wakizugumza baadhi ya wananchi wa maeneo hayo walimshukru Viongozi wa Jimbo hilo kwa maamuzi yao ya ujenzi wa barabara hiyo kwani itasaidia wanafunzi kupata njia ya uhakika kuwahi skuli sambamba na wakulima kupata njia ya uhakika ya kusafirisha mazao yao.
Dk. Mabodi alifanya harambee ya kuchangia ujenzi wa Ofisi ya kisasa ya CCM katika eneo la Kikungwi pamoja na kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa mashindano ya mpira wa miguu ya Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja.