TIMU ya taifa ya Argentina imetwaa ubingwa wa michuano ya Copa America baada ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Brazil Alfajiri ya leo Uwanja wa Jornalista Mario Filho, au Maracana Jijini Rio de Janeiro.
Bao pekee la Argentina limefungwa na Ángel di Maria dakika ya 22 akimalizia pasi ya Rodrigo de Paul, hilo likiwa taji la kwanza kwao la michuano mikubwa baada ya miaka 28.
Furaha kubwa ilikuwa kwa Nahodha, Lionel Messi ambaye ametwaa taji la kwanza la Copa America na kwa ujumla la kwanza kubwa akiwa na timu ya taifa.
Hali ilikuwa tofauti kwa Nahodha wa Brazil, Neymar Junior aliyeangua kilio uwanjani akimwaga machozi kwa huzuni baada ya kushindwa kuisaidia Brazil kutwaa taji nyumbani.
Pamoja na huzuni hiyo, Neymar anayechezea Paris Saint-Germain ya Ufaransa kwa sasa alijikongoja na kwenda kumpongeza Messi, mchezaji mwenzake wa zamani wa Barcelona.
Hilo linakuwa taji la 15 Argentina baada ya awali kulibeba 1921, 1925, 1927, 1929, 1937, 1941, 1945, 1946, 1947, 1955, 1957, 1959, 1991 na 1993, wakati Brazil imetwaa mataji tisa tu 1919, 1922, 1949, 1989, 1997, 1999, 2004, 2007 na 2019.