Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiangalia ramani ya majengo ambayo hayajakamilika na ķusikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari Dkt. Magreth Kyewalyanga alipotembelea Taasisi hiyo kuona maendeleo ya ujenzi wa majengo mbalimbali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akitoa maelekezo kuhusu namna ya ukamilishaji wa miundombinu ambayo haijakamilika kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu, Zanzibar Dkt. Magreth Kyewalyanga alipotembelea Taasisi hiyo.
Mbunge wa Kiembe Samaki Mhe. Mohammed Maulid akizungumza katika kikao cha waziri na watumishi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari, wakati Waziri alipofanya ziara katika Taasisi hiyo Buyu, Zanzibar
Muonekano wa moja ya majengo ya Taasisi ya Sayansi za Bahari yaliyopo Buyuni Zanzibar yaliyokamilika kujengwa
…………………………………………………………………
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeahidi kukamilisha ujenzi wa majengo katika Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyopo Buyu, Zanzibar
Akizungumza baada ya kukagua chuo hicho Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Wizara kupitia mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu tayari imeshatenga zaidi ya Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika Taasisi hiyo.
Waziri Ndalichako amesema mbali ya fedha hizo Wizara imeshaanza kufanya mapitio ya miradi yake ili kuona namna ya kupata fedha za kumalizia ujenzi wa majengo ambayo tayari misingi yake imeshajengwa na imekaa muda mrefu bila kukamilishwa.
“Mbali ya kutenga fedha za ujenzi wa mabweni, lakini mimi na Katibu Mkuu tulishaanza kufanya mapitio miradi tuliyonayo katika wizara kuona inawezaje kusaidia kukamilisha ujenzi wa majengo yote yaliyoishia katika hatua ya msingi ambayo ni muhimu katika kukamilisha mafunzo,” amesema Profesa Ndalichako.
Waziri huyo amesema kamwe Serikali haiwezi kuona fedha zilizotumika kujenga misingi hiyo zinapotea bure kwa kuwa hakuna fedha za kukamilisha ujenzi. Amesema matamanio yake ni kuona majengo hayo yanaanza kujengwa katika mwaka 2021/22 na kukamilika mwaka 2022/23 ili madhumuni ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo yafikiwe ikiwa pamoja na kutekeleza sera ya uchumi wa bluu.
Aidha, ameupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kuanza masomo pamoja na kuwa na changamoto mbalimbali, amezisitiza kuwa chuo hicho kinatekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan juu ya kuandaa vijana wenye ujuzi ambapo Taassisi hiyo ina Programu za mafunzo mbalimbali ambayo yanatoa ujuzi katika tasnia ya Sayansi ya Bahari.
Naye Mbunge wa Kiembe Samaki ambapo Taasisi hiyo ipo Mhe. Mohammed Maulid amemshukuru Waziri kwa kufika katika Taasisi hiyo ambayo ni tegemeo kubwa kwa taifa katika kuandaa wataalamu wa sayansi ya majini ambao wataiwezesha kufanikisha uchumi wa bluu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari Dkt.Magreth Kyewalyanga amemwambia waziri kuwa ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu iliyo kwenye hatua ya msingi zinahitajika kiasi cha shilingi bilioni saba na milioni mia tano.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Serikali ya wanafunzi DARUSO Frank Buluma amesema Taasisi hiyo imewasaidia wao kama vijana kupata fursa ya kupata elimu ya Sayansi ambayo itawawezesha kushiriki katika kukuza uchumi kupitia uchumi wa bluu. Ametoa wito kwa vijana kujiunga na chuo hicho ambacho kitawawezesha kupata elimu itakayowasaidia kujiajiri katika eneo jipya la ajira.
Taasisi ya Sayansi za Bahari, inatoa mafunzo katika ngazi umahiri, uzamivu na shahada za awali, kufanya tafiti na kutoa ushauri katika maeneo mbalimbali ya Sayansi ya Bahari.